Unapotaka kutumia gari lako kwa safari yoyote ile, iwe ya umbali mrefu au ya umbali mfupi, unatakiwa kuhakikisha kuwa gari lako liko salama ili liweze kukufikisha huko unapokwenda salama.
Achana na ufundi mkubwa wa kitaalamu, tunachozungumzia hapa ni vitu vichache vya kawaida ambavyo unatakiwa kuvikagua kila asubuhi kabla ya safari.
Haijalishi gari lako usiku wakati umelifikisha nyumbani lilikuwa kwenye hali gani, unatakiwa kulikagua kabla ya safari. Epuka sana tabia ya kuingia kwenye gari, ukaliwasha na kuondoka bila kuhakikisha kama liko salama kwani unaweza kupata matatizo ukiwa njiani na kushindwa kufika unapokwenda, au ukapata ajali inayoweza kukupelekea kupata majeraha au kifo.
Katika makala ya leo tutachambua vitu vitano unavyotakiwa kuvikagua kila siku asubuhi kabla ya kuliwasha gari lako kwa ajili ya safari iwe ya mbali au karibu.
Maji ya ‘wiper’
Kila siku kabla ya kuliwasha gari lako ukiwa nyumbani unashauria kukagua maji ya wiper (zinazotumika kusafisha vioo) ili kuhakikisha yapo ya kutosha.
Maji haya hutumika kusafisha kioo cha mbele cha gari lako au nyuma (kwa baadhi ya magari) endapo kitachafuliwa kwa namna yoyote. Mfano umepita sehemu yenye vumbi kali, au umerushiwa maji kwenye kioo na gari jingine wakati ukiwa kwenye mwendo.
Jiulize utakuwa katika hali gani endapo umerushiwa maji machafu kwenye kioo halafu kwenye gari lako hauna maji ya wiper. Endapo utawasha wiper za gari ili kusafisha kioo cha mbele, hazitosafisha na badala yake zitazidi kuusambaza uchafu na kukufanya ushindwe kuona vizuri barabarani. Hapo hutoweza kuona mbele na kutokana na mshtuko mkubwa utakaokuwa nao wakati huo, uwezo wa kulitawala gari lako utakuwa ni mdogo na hivyo kupelekea ajali.
Kiasi cha upepo (pumzi) katika tairi
Kila aina ya matairi ya magari huwa na kiwango fulani cha upepo yanayotakiwa kuwa nacho, hivyo kabla ya safari ni vyema kuangalia kiwango cha upepo kama kipo cha kutosha na kama kipo chini ya kiwango unapaswa uongeze.
Labda hujui hatari ya kuendesha gari ambalo upepo wa tairi ni mdogo. Kwanza, uwezekano wa gari lako kuyumba na kutoka nje ya barabara ni mkubwa sana jambo ambalo linaweza kusababisha ajali. Pili, gari ambalo matairi yake yana upepo kidogo litatumia mafuta mengi ili liweze kwenda kasi tofauti na matairi ambayo yana upepo katika kiwango kinachotakiwa.
Fahamu jinsi ya kutambua uwezo wa spidi ya matairi ya gari lako
Hatari nyingine ya kuendesha gari ambalo upepo wa tairi ni mdogo ni kuharibu rimu za gari kwani zitaweza kushuka chini hadi kukwangua barabara. Upepo ukiwa mdogo kwenye tairi, hatari nyingine ni kuwa joto la tairi liitaongezeka kwa sababu msuguano kati yake na barabara utakuwa ni mkubwa na eneo kubwa la tairi litakuwa limelala juu ya barabara tofauti na kawaida.
Hakikisha upepo wa tairi ya gari unakuwa katika uwiano sawa lisiwepo tairi lenye upepo mwingi kuliko jingine labda tu pale ambapo ndio mfumo unaotakiwa kama ilivyo kwa magari mengi ambayo matairi ya nyuma huwa na upepo mwingi kidogo kuliko ya mbele.
‘Coolant’
Kwenye gari, coolant kama inavyofahamika kwa jina la kiingereza ni kimiminika ambacho hutumika katika kupoozea injini ya gari lako linapokuwa linatumika. Kutokana na gharama kubwa ya vimiminika hivyo, watu wengi wakishavununua huchanganya na maji na kisha kuviweka katika rejeta ya gari, lakini kiusahihi vimimika hivyo vilitakiwa kuwekwa kwenye rejeta bila kuchanganywa na maji.
Unasahuriwa kuweka coolant kwenye rejeta bila kuchanganya na maji kwa sababu itakaa muda mrefu bila kubadilisha tofauti na unapochanganya na maji ambapo gari litachemsha lakini kumbuka kuwa kiwango cha maji kuchemka (boiling point) ni kidogo ukilinganisha na ‘coolant’. Maji yanapochemka huwa mvuke na hivyo itakulazimu kila mara kuongeza maji katika rejeta.
Faida nyingine ya kutumia coolant badala ya maji ni kuwa, yenyewe husaidia kuzuia rejeta ya gari isipate kutu, hivyo unapoweka maji, unaharibu rejeta kwani litashika kutu.
Taa za gari
Wengine watasema, mimi nakwenda hapo mbele tu na ni mchana, sasa kuna haja gani ya kuanza kukagua taa kama zinafanya kazi angali sitazitumia? Hapa hatuzungumzii taa za mbele zinazokusaidia kuona wakati wa usiku, bali taa zote kwenye gari lako lazima ziwe zinafanya kazi kwa hata kama ni mchana kuna nyingine zinatumika.
Fahamu aina na matumizi ya taa mbalimbali za kwenye gari
Kuanzia taa za mbele, taa za kuegesha gari, taa za ukungu, taa za ishara, taa za breki, taa za kwenye namba ya gari zote zinatakiwa ziwe zinafanya kazi.
Umuhimu wa kuhakikisha taa hizi zinafanya kazi ni ili kurahisisha mawasiliano unapokuwa barabarani, kwa mfano ukitaka kuingia upande kushoto utatakiwa kutoa ishara, au kama kwenye gari umebeba mgonjwa anayehitaji kuwahishwa hospitali utatakiwa kuwasha taa za kuashiria hatari (hazard) ili kutoa ishara kwa watumiaji wengine.
Lakini pia ni kosa kisheria endapo uatakamtwa hata kama ni mchana unaendesha gari ambalo taa zake hazifanyi kazi kwani unaweza kusababisha ajali kwa watumiaji wengine wa barabarani.
Kilainishi cha injini (engine oil)
Kilainishi hiki huwa hakiishi haraka kwamba utatakiwa kuongeza kila siku asubuhi, ila umuhimu wa kukagua kila mara ni kuweka kujua kiasi kilichopo na ubora wake kama imefika wakati kubadilishwa au la.
Matumizi makubwa ya kilainishi hiki ni kuzuia vyuma ndani ya njini kusagana kutokana na kuwapo msuguano wakati gari likifanyakazi, lakini pia inaisaidia injini kufanya kazi kwa urahisi zaidi.
Vitu hivyo vikiwa sawa ndani ya gari lako, vitakuhakikishia usalama wa safari yako. Jambo jingine muhimu unalotakiwa kufanya, kabla ya kuanza safari na gari lako, liwashe angalau kwa dakika 3 na uliache likiwa linaunguruma ili lijiweke sawa tayari kwa safari.
Kumbuka kuwa na kiasi kidogo cha fedha mfukoni ambacho kitakusaidia endapo tatizo lolote litatokea. Gari lako linaweza kuwa salama lakini ukasababishiwa matatizo na gari jingine.
Post a Comment
Post a Comment