Watu wengi sana hasa wanawake hupata wakati mgumu kuendesha gari lenye mfumo wa ‘manual transmission’ kwani magari haya humtaka dereva kufanya kila kitu mwenyewe tofauti na ‘automatic transmission’ ambalo baadhi ya mambo hufanya lenyewe na hivyo kumuachia dereva majukumu machache tu.
Changamoto inayowakumba wengi hata ambao wamekuwa wakiendesha gari la manual transmission kwa muda mrefu ni namna ya kuondoka kwenye eneo lenye mwinuko pasi na gari kurudi nyuma ambao linaweza kusababisha madhara kama kuna gari jingine limeegeshwa nyuma.
Kwa ufupi tutaangalia njia tatu za kukusaidia kuweza kuondoa gari lako katika sehemu yenye mwinuko bila kusababisha madhara au gari lako kurudi nyuma.
Njia ya kwanza ni kutumia breki ya dharura.
Breki hii watu wengi huifahamu kama breki mkono (hand break) kwa sababu kwenye magari mengi huwekwa kwa kutumia mkono, lakini ni vyema kuelewa kuwa kuna magari mengine breki hii huwekwa kwa kutumia mguu.
Namna ya kutumia breki hii kuondoa gari lako kwenye kilima kwanza hakikisha breaki yako ya dharura umeiweka halafu unaweza kuliwasha gari lako, kanyaga pedo ya ‘clutch’ baada ya hapo, ingiza gia namba moja, halafu kanyaga mafuta kiasi huku ukiiachia pedo ya clutch taratibu. Baada ya sekunde utaona gari kama linaanza kutikisika na ukishuka au kuitoa breki yako ya dharura, gari litaondoka bila kurudi nyuma.
Mambo ya msingi ya kuzingatia hapa ni kuwa, ukubwa au mwinuko wa kilima ndio utaamua ni mafuta kiasi gani uweke. Kadiri kilima kinavyoinuka zaidi, ndiyo mafuta yakavyohitajika kwa gari lako kuondoka bila matatizo. Lakini pia hakikisha unapoachia clutch yako, unaiachia taratibu na si kwa ghafla kwani gari litazima.
Njia ya pili ni kutumia breki na kichapuzi (accelerator) kwa wakati mmoja.
Njia hii ni rahisi pia lakini inakutaka kuwa makini na mguu wako kuwa mwepesi kiasi unapoitumia kuondoa gari lako kwenye kilima bila kuleta madhara.
Unachotakiwa kufanya hapa ni, kuwasha gari lako, kisha kanyaga clutch na kuweka gia namba moja, ikifuatiwa na breki kisha ondoa breki yako ya dhararu (hand break) ambapo sasa gari litakuwa likiitegemea breki yako uliyokanyaga kwenye mguu. Hivyo unatakiwa kuwa makini kwani miguu yako ikiwa mizito kidogo unaweza kusababisha madhara.
Baada ya kutoa breki ya mkono, mguu wako wa kulia ambao umekanyaga breki uweke kwa upande (kama pichani hapo juu) uwe juu ya pedo ya breki na accelerator kwa wakati mmoja lakini wakati huo sehemu ya kisigino cha mguu wako kinatakiwa kiwe bado kimeshikilia breki, wakati sehemu ya vidole ikiwa juu ya pedo ya mafuta. Utakachotakiwa kufanya ni kuachia pedo ya clutch taratibu huku ukiinua kisigino chako na wakati huo huo sehemu ya mbele ya mguu wako ukiminya pedo ya mfuta, na gari litaanza kuondoka.
Muhimu, hakikisha miguu yako inafanyakazi kwa ushirikiano sawa kwani, mfano, ukiinua kisigino bila kubonyeza pedo ya mafuta gari litarudi nyuma kwa kukosa nguvu ya kulipeleka mbele, au ukiminya pedo ya mafuta na breki kwa wakati mmoja, gari litaishia kupiga kelele bila kwenda popote, hivyo hakikisha miguu yako inawasiliana.
Njia ya tatu ni kutumia uwiano wa pedo ya clutch na mafuta.
Njia hii hutumiwa mra nyingi na watu ambao ni wazoefu sana katika kuendesha magari ya manual transmission ambayo inamtaka dereva kuweza kuweka uwiano sawa wa kukanyaga pedo ya clutch na mafuta kwa wakati mmoja.
Kinachofanyika katika njia hii ni kuwa, dereva akiwasha gari lake, ataingiiza gia wakati mguu wake upo kwenye breki ili aweze kuondoa breki ya mkono bila gari kurudi nyuma. Baada ya hapo dereva atahamisha mguu wake kutoka kwenye breki kwa haraka na kuuhamishia kwenye pedo ya mafuta wakati huo huo ataachia cluth kwa kiasi fulani ili aweze kukanyaga mafuta yatakayoruhusu gari kuondoka.
Ukiitumia njia hii, hakikisha kuwa hauruhusu mafuta mengi kuingia kwenye injini wakati unahamisha mguu wako kwa haraka, au kuachia clutch ghafla hadi mwisho kwani gari litashtuka na kuzima.
Njia hii inaaminika kuwa ni ngumu zaidi kuliko mbili zilizotangulia kwani inamhitaji dereva kufanya maamuzi kwa haraka zaidi na kuhakikisha kuwa yanakuwa ya ufasaha.
Post a Comment
Post a Comment