Sambamba na kutoka kwa miwani hii mpya ya kwanza ya aina yake, Snapchat wamebadilisha jina la kampuni yao kuwa Snap Inc.— uamuzi utakaowafanya waweze kujihusisha na kufanya shughuli nyingi zaidi zinazohusu teknolojia. Baada ya miezi kadhaa ya kuuza miwani hizi kwenye maduka maalumu tu, sasa Snap imeanza kuziuza mtandaoni miwani hizi zinazorekodi video.
Miwani hii ina lenzi maalumu yenye uwezo mkubwa wa kurekodi video. Hii inasaidia video hizo ziweze kuonekana vizuri kwenye simu yoyote. Pia inafanya kazi ya kurekodi video zako binafsi – hata kama hutaki kuzitumia kwenye Snap, pia ni fasheni nzuri, na ni njia ya mtandao wa Snap kuwa na video ambazo zina ubora ambao haupatikani popote.
Kwa uamuzi huu wa kufanya idadi maalumu ya miwani hizi kuuzwa kwa njia ya mtandao kwa wateja wa nchini Marekani badala ya kusubiri kwenye maduka machache tu, Snap inaziweka miwani hizi majaribuni. Swali kubwa ni je, watu wanahitaji kweli miwani hizi au uamuzi wao wa kuziuza kwenye maduka machache ilikuwa ni wa makusudi kuwafanya watu wajae shauku ya kuzinunua watakapoziachia kama hivi?
Maduka haya machache yalipoanza kuziuza kwenye majiji makubwa, watu wengi walionekana kupanga foleni kubwa wakisubiri kuzinunua. Wengine wakaamua kununua zaidi ya moja na kuziuza tena kwenye mtandao wa eBay kwa bei ya mpaka dola 900, sawa na shilingi miloni mbili za Tanzania. Bei hizi za juu sasa zimeshuka kwa kiasi kikubwa sana, kwakuwa uchache wake sasa sio dili tena. Kwa sasa unaweza kuzipata kwa dola 130, sawa na shilingi 290,000 za Tanzania na Snap wanaomba dua kila kukicha zipokelewe na watu wengi duniani ili uwekezaji wao uwe na maana kubwa kibiashara.
Wiki hii Snap wanaanza kuuza hisa za kampuni hiyo na inahitajika kuwashawishi wawekezaji ambao wengi hawana uhakika kwamba kuwekeza kwenye kampuni hiyo ni uamuzi wa busara kibiashara ama ni sawa na kutupa pesa zao. Jarida la Wall Street limeripoti kuwa kwenye taarifa za kuiweka kampuni hiyo katika soko la hisa, “miwani hizo zimetajwa mara 45 na katika hizo, mara 18 zimetajwa kwamba ndio uwekezaji mkubwa uliowahi kufanywa na kampuni hiyo.”
Watafiti wanaamini kuwa uamuzi wa kuuza miwani hizi mtandaoni unatokana na kuporomoka kwa shauku ya watu. Maduka maalumu yaliyokuwa yanaziuza miwani hizi hazijazi watu tena kama ilivyotegemewa na viongozi wa kampuni hii.
Wakati kampuni ya Facebook inaamua kutangaza uamuzi huu wa kuuza hisa ilikuwa imeshaanza kutengeneza faida ya dola bilioni moja za Marekani, sawa na zaidi ya trilioni mbili za Tanzania, na toka kipindi hicho imekuwa kuwapa faida kubwa wawekezaji wake. Kwa upande wa pili, kampuni ya Twitter ilifikia uamuzi huo wakati ikiwa ipo kwenye hasara na mpaka sasa wanaendelea kupata hasara. Uamuzi huu wa Snap kutengeneza vifaa vya teknolojia yawezekana ukawa wa maana kibiashara kwakuwa mpaka sasa inachukuliwa kama mtandao wa kijamii tu.
Jamaa atengeneza ndege YAFANIKIWA KURUKA
Post a Comment
Post a Comment