IKIWA ni takribani siku 13 tangu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na Jeshi la Polisi kuanza kampeni ya kukamata na kutangaza majina ya watuhumiwa wa biashara ya dawa za kulevya, baadhi ya watumiaji wa dawa hizo (mateja), wamelalamika kuadimika kwa bidhaa hiyo na ikipatikana bei yake inakuwa juu mara mbili.
Taarifa hizo ambazo ni njema kwa viongozi wanaoendesha vita hiyo iliyotangazwa na Rais Dk. John Magufuli alipokuwa akizindua Bunge la 11, zilipatikana baada ya gazeti hili kutembelea baadhi ya maeneo maarufu Dar es Salaam wanapopatikana watumiji wa dawa hizo.
Taarifa zilizopatikana kutoka kwa watumiaji hao, zilisema bei ya dawa hizo za aina ya heroin kwa kete moja, imepanda mara tano zaidi ya bei ya awali iliyokuwa ikiuzwa kabla ya kuanza kwa kamata kamata. Tumeacha kutaja bei kwa sababu za kitaalamu.
Walisema licha ya kupanda kwa bei hiyo, hata wauzaji sasa hawamuuzii mtu wasiyemjua kwa hofu ya kukamatwa.
Katika kituo cha Manyanya Kinondoni, baadhi ya mateja walisema kuwa kwa sasa tangu sakata la kuwakamata wauzaji, waingizaji na watumiaji, unga umepanda bei kutokana na kuadimika kwani wauzaji wanauza kwa kujificha.
Mmoja wa mateja hao aliyejitambulisha kwa jina moja la Aisha, alisema kwa sasa si rahisi kupata unga kwa sababu wauzaji wanauza kwa kujificha na kama ukipatikana bei yake imepanda maradufu.
“Ni shida kupata unga sasa hivi maana waliokuwa wanatuuzia wanajificha ili wasikamatwe, kwahiyo ukibahatika kuupata utauziwa kwa bei ya juu kwa sababu siku za nyuma kete ulikuwa unapata kwa Sh 1,000 hadi 2,000 lakini sasa hivi unaanzia 3,500 hadi 5,000.
“Mfano kulikuwa na muuzaji hapo upande wa pili wa barabara, lakini amekamatwa na hakuna tena dawa hapo,” alisema Aisha.
BADO WAPO
Hata hivyo, mateja hao waliendelea kuwapo katika maeneo hayo tofauti na ilivyodaiwa kuwa wakilewa watakamatwa na kupelekwa kituo cha polisi ili wawataje wanaowauzia.
Katika vituo vya daladala vya Mwananyamala Hospitali, A, Tandale, Magomeni Kagera, Kinondoni Mkwajuni na Studio, mateja walikuwapo japo walionekana kuwa na wasiwasi mkubwa.
WAOMBA KUPELEKWA SOBER HOUSE
Mmoja wa mateja waliokuwapo katika kituo cha daladala cha Magomeni Kagera aliyejitambulisha kwa jina moja la Juma, alisema wanaiomba Serikali kuwasaidia kwa kuwapeleka katika vituo vya tiba za waathirika (sober house) ili wakapate matibabu kwa kuwa baadhi yao wameanza kupata madhara kutokana na kuadimika kwa dawa hizo.
“Tunaiomba Serikali itusaidie kwa kuwa wenzetu ambao wanakosa ‘unga’ wanapata shida sana kwa kutapika na kuharisha na hali zao si nzuri,” alisema.
WAFANYABIASHARA WAPONGEZA
Baadhi ya wafanyabiashara katika maduka yaliyo jirani na vituo vya daladala, wamesema hatua iliyochukuliwa na Serikali kupambana na dawa za kulevya itapunguza wizi katika mitaa yao.
Mmoja wa wafanyabiashara hao aliyejitambulisha kwa jina la Mama Winnie katika kituo cha Mwananyamala A, alisema kuwa wimbi la wizi lilikuwa likiongezeka siku hadi siku kutokana na mateja kutafuta fedha za kuvutia.
“Hapa tulikuwa tunaibiwa sana na unaweza kuletewa nguo mbichi iliyoanuliwa kwenye kamba na kuuziwa kwa bei rahisi tofauti na bei yake halisi, ili mradi tu apate fedha ya kununulia unga,” alisema Mama Winnie.
Post a Comment
Post a Comment