Ofisi ya biashara wilaya ya Makete imekiri kuwa kuna upotevu wa mapato katika stendi mpya ya Tandala na stendi ya Iwawa kutokana na kuwepo kwa mashine moja tu ya (EFD) kila kijiji,hali inayowafanya wanaosimamia mapato kwenye maeneo hayo kutumia mashine hizo sehemu zaidi ya moja,hivyo kupishana na magari ya abiria.
Kauli hiyo imetolewa na afisa biashara wilaya ya Makete Bw.Edonia Mahenge alipokuwa akizungumza nasi kuhusu stendi hizo mbili zinavyochangia mapato katika halmashauri ya wilaya ya Makete.
Aidha Bw.Mahenge amesema stendi zote mbili zimekuwa zikiendeshwa kwa mujibu wa sheria huku akisema kuwa kulikuwa na changamoto kubwa katika stendi mpya ya Tandala ambapo kwa sasa changamoto hizo zimefanyiwa kazi.
Bw.Mahenge ameongeza kuwa hivi karibuni ofisi ya TANROADS mkoa wa Njombe ilitoa notisi kuwa kuanzia tarehe 21 ya mwezi wa tatu mwaka huu kwamba miundombinu yote iliyo kwenye hifadhi ya barabara iwe imeondolewa,hivyo ana imani kuwa biashara nyingi zitahamia stendi mpya.
Amewahakikishia wafanyabiashara na wananchi wote kwa ujumla kuwa miundombinu ya stendi mpya ya Tandala kwa sasa ni rafiki kwani huduma zote muhimu zinapatikana.
Afisa biashara huyo pia amesema kwa sasa halmashauri haina fedha za kujenga vibanda maeneo ya stendi Hiyo hivyo wamewaachia wananchi fursa hiyo na baadae wataangalia namna bora ya kufanya.
Post a Comment
Post a Comment