Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imezitaka shule zote zilizowataka wazazi/walezi kuwahamisha watoto wao kwa kigezo cha kutofikia wastani wa ufaulu, kufuta agizo hilo na kuendelea na wanafunzi hao bila masharti yoyote.
Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Kaimu Kamishna wa Elimu, Nicolas Buretta imeeleza kuwa wazazi wenye wanafunzi waliorudishwa nyumbani kwa sababu hiyo wahakikishe wanawarudisha kwenye shule walizokuwa wakisoma ili waendelee na masomo yao kama kawaida.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Serikali imefikia hatua hiyo baada ya kubainika kuwa bado kuna shule nyingi za msingi na sekondari hususani zisizo za Serikali na zaidi za kidini zinazoendelea kukaririsha, kuhamishia shule nyingine au kuwafukuza wanafunzi kwa kigezo cha kutofikia alama za ufaulu zilizowekwa na shule hizo jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Badala ya shule hizo kuchukua hatua hiyo, wizara hiyo imesema, “...Ziwe na utaratibu wa kuinua viwango vya taaluma kwa wanafunzi wenye ufaulu mdogo na hivyo siyo ruhusa kukaririsha darasa wanafunzi kwa kigezo cha kutofikia wastani wa ufaulu uliowekwa na shule. Ikitokea, ni lazima kufanya hivyo, taratibu zilizopo zifuatwe.”
Taarifa hiyo imeelekeza wadhibiti ubora wa shule, kanda na wilaya, maofisa elimu wa mikoa na wilaya kusimamia utekelezaji wa agizo hilo katika maeneo yao.
“Shule yoyote itakayokiuka maagizo hayo itachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria zilizopo.”
Post a Comment
Post a Comment