Na Ahmad Mmow, Lindi.
Mkuu wa wilaya ya Lindi ameitaka kampuni ya ujenzi ya scorpion Limited itakayo jenga miradi ya maji ya Nangaru Corridor na Mkwajuni- Nanjime imalize kazi kwa wakati na ijenge kwa viwango sahihi.
Mkuu wa wilaya(DC) Ndemanga alitoa agizo hilo jana katika vijiji vya Nangaru na Mkwajuni kwa nyakati tofauti wakati wa hafla ya kumkabidhi mkandarasi huyo maeneo ya mradi.
Ndemanga alisema hatokubali kusikia sababu zozote ambazo zitasababisha mkandarasi huyo kushindwa kumaliza na kukabidhi kwa wakati miradi hiyo ambayo itagharimu shilingi bilioni 2,369,121,784.34 hadi kukamilika.
Aidha Ndemanga amemtaka mkandarasi huyo ajenge kwa viwango sahihi kama inavyoonesha kwenye mikataba ya kazi hizo ambayo ilisainiwa jana katika vijiji hivyo.
" Tabia ya kuleta na kutumia vifaa visivyo na ubora sitaki. Utaleta bomba, kesho zitapasuka, sitaki kusikia bradha," alisisitiza Ndemanga.
Amemtaka azingatie kikamilifu miongozo na maelekezo yaliyopo ndani ya mikataba. Kwani hatakuwa tayari kupokea ikiwa imejengwa chini ya kiwango.
Aidha Ndemanga aliwaonya viongozi wa serikali za vijiji na kamati za watumia maji waepuke migogoro baina yao. Kwani baadhi ya viongozi wa serikali za vijiji na kamati za watumia maji wanagombana na kusababisha miradi kukosa usimamizi sitahiki. Hivyo kukwamisha juhudi na nia njema ya serikali kwa wananchi wake.
Post a Comment
Post a Comment