Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe leo asubuhi ametangaza kusitisha uteuzi wa Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Dionis Malinzi pamoja na wajumbe wote wa Baraza hilo ambapo kuanzia sasa mpaka itakapotangazwa uamuzi tofauti, majukumu yaliyokuwa yanafanywa na BMT yatafanywa na sekretarieti ya Baraza hilo kwa ushirikiano wa karibu na Wizara yake.
Waziri Mwakyembe ametangaza kusitisha uteuzi wa Mwenyekiti na wajumbe wote wa Baraza hilo kwa mujibu wa mamlaka aliyopewa na Sheria ya BMT namba 12 ya mwaka 1967.
Akitangaza uamuzi huo kwenye ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo, Dkt. Mwakembe alisema:
Agizo la Mheshimiwa Waziri Mkuu limekuja kipindi muafaka kwani mara baada ya uteuzi wangu kuongoza Wizara hii, niliitisha kikao na BMT kujielimisha kuhusu wajibu wa kisheria, changamoto zinazolikabili Baraza hilo na hali ya uhuria uliopitiliza katika uongozi na uendeshaji wa michezo karibu yote nchini.
Pamoja na BMT kulalamikia sana suala la uhaba wa pesa kuwa kikwazo kikubwa kinachokwamisha utendaji kazi wake, Wizara ililiona zaidi hitaji la utashi, dhamira na kujituma kuliko pesa katika kutatua sehemu kubwa ya udhaifu uliotamalaki tasnia ya michezo. Mifano michache:
Viongozi wa michezo kushika zaidi ya nafasi moja ya uongozi (katika mchezo mmoja); ushiriki wa wanamichezo wa Tanzania nje ya nchi bila kuitaarifu BMT; mapromota wa mchezo wa ngumi nchini kuendesha shughuli zao bila kusajiliwa; chaguzi za vyama vya michezo kugubikwa na ubabe na rushwa; katiba na kanuni za vyama vya michezo kukosa uhakiki kubaini upungufu kuhusu masuala ya fedha; tuhuma za rushwa, ubadhirifu, upendeleo, maamuzi ya kibabe ya wazi kabisa kutofuatiliwa na kufanyiwa kazi, n.k.
Baraza la Michezo la Taifa limeundwa kwa mujibu wa sheria ya Bunge na. 12 ya mwaka 1967 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 1971. Jukumu kubwa la Baraza ni kuendeleza michezo nchini kwa kushirikiana na vyama vya michezo. Chini ya Sheria hiyo na kanuni zake (na. 441 za 1999), Waziri mwenye dhamana na michezo ana mamlaka ya kuteua wajumbe wanaounda Baraza kadiri atakavyoona inafaa, pamoja na Mwenyekiti wake.
Kipindi kirefu tasnia ya michezo imegubikwa na migogoro ya mara kwa mara ambayo imechangia sana kudumaza maendeleo ya michezo katika nchi yetu. Serikali ya awamu ya tano ilitarajiwa kwamba kupitia BMT, migogoro hiyo ingeweza kupatiwa ufumbuzi wa kudumu. Kwa mujibu wa Sheria iliyoanzishwa BMT, Baraza limepewa jukumu la kushughulikia masuala yote yanayohusu michezo ikiwa ni pamoja na weledi, amani, utulivu na utawala bora katika tasnia ya michezo.
Pamoja na kutambua juhudi zilizofanywa na Baraza toka liteuliwe mwaka 2015, naamini kuwa changamoto zilizo mbele yetu katika tasnia ya michezo, kasi ya mageuzi katika Serikali ya Awamu ya Tano pamoja na matarajio ya haraka waliyonayo wananchi kuiona tasnia hii ikionesha tija, vinahitaji mikakati mipya na nguvu mpya. Hivyo basi, nimeamua leo tarehe 10 Julai, 2017, kwa mamlaka niliyopewa na Sheria ya BMT na. 12 ya 1967 (kama ilivyofanyiwa marekebisho na Sheria na. 6 ya 1971) pamoja na kanuni zake za 1999, kusitisha uteuzi wa Mwenyekiti pamoja na wajumbe wote wa BMT kuanzia leo 10 Julai 2017.
Sekretarieti ya Baraza itaendelea kufanya kazi katika kipindi hiki kwa kushirikiana kwa karibu na Wizara wakati taratibu za kumpata Mwenyekiti na wajumbe wapya zikiendelea kufanyika kwa mujibu wa Sheria”
WASANTE KWA KUTEMBELEA MTANDAO WETU!!
W
Post a Comment
Post a Comment