Mbunge wa Hai mkoani Kilimanjaro, Freeman Mbowe amefugua kesi mahakamani dhidi ya Mkuu wa Wilaya ya Hai, Dk Gelasius Byakanwa akimdai fidia ya zaidi ya Tsh milioni 549.3
Mbowe kupitia Kampuni ya Kilimanjaro Veggies Ltd amefungua kesi hiyo katika Mahakama Kuu Kanda ya Moshi akidai kiasi hicho cha fedha kufuatia kiongozi huyo kuongoza uharibifu wa miundombinu ya umwagiliaji katika shamba lake la mbogamboga Juni 19 mwaka huu.
Katika hati ya mashtaka ya kesi hiyo, Mbowe amemshtaki Dk Byakanwa kama mtu binafsi akimtuhumu kuingia kinyemela kwenye shamba lake na kufanya uharibifu wa mali.
Kesi hiyo ambayo ipo chini ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Moshi, Aishael Sumari, ilifunguliwa Juni 30, na ina mashauri mawili ambayo ni shauri la ardhi namba 20/2017 na maombi madogo namba 51/2017.
Katika maombi madogo, mshtaki anaiomba mahakama iweke zuio la kudumu kwa mshtakiwa kutoingilia tena shughuli za Kampuni ya Kilimanjaro Veggies Ltd ambayo inafanyakazi zake katika Kijiji cha Nshara, Kata ya Machame Kaskazini, wilayani Hai, Mkoa wa Kilimanjaro.
Aidha, katika shtaka lingine, mshtaki anaiomba mahakama imuamuru mshtaki alipe fidia maalumu Tsh 549.3 inayotokana na uharibifu wa mali, usumbufu walioupata pamoja na hasara ya KVL. Kampuni hiyo inaiomba mahakama imuamuru mshtakiwa pia, alipe riba ya 25% ya fedha hizo pamoja na kulipa gharama za uendeshaji kesi hiyo.
Jaji Mfawidhi alitaka mshtakiwa apelekewe nyaraka za kesi hiyo na awe amewasilisha majibu kabla ya usikilizwaji wa maombi Julai 17.
Post a Comment
Post a Comment