Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema kuwa, kimepokea kupitia vyombo vya habari taarifa za tukio la mwandishi wa habari wa TBC kushindwa kutimiza wajibu wake katika ofisi za Makao Makuu yake zilizopo Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
CHADEMA imesemema, tukio hilo halikufanywa kwa maelekezo ya kiongozi yeyote na kama chama, hawajawahi na hawana sera wala msimamo wa kubagua chombo chochote cha habari.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa CHADEMA, John Mrema wamesema kwamba, katika hatua za awali wanafanyia uchunguzi tukio hilo ili kuweza kubainisha nini hasa kilitokea katika siku hiyo na wanategemea kupata ushirikiano kutoka kwa mwandishi husika katika uchunguzi wao.
Aidha, taarifa hiyo kutoka CHADEMA aliwahakikishia waandishi wote wa habari kuwa wataendelea kuwa salama katika matukio yote ambayo yatakuwa yakifanywa na chama hicho na watapata ushirikiano unaostahili.
“Baada ya uchunguzi wetu kukamilika tutatoa taarifa kamili juu ya tutakachokuwa tumebaini na hatua tutakazochukua. Sisi tunaamini katika uhuru wa vyombo vya habari, uhuru wa waandishi wa habari na haki ya kupata na kutoa habari/taarifa kuwa ni nguzo kuu katika kujenga taifa la kidemokrasia na hatimaye kufikia maendeleo ya kweli.”
Katika kudhihirisha kwa vitendo kuwa wanathamini uhuru wa habari na uwajibikaji, Mrema alisema, CHADEMA ni taasisi ya kwanza ya kisiasa iliyotia saini na kukubaliana na Azimio la Dar es Salaam Juu ya Uhuru wa Uhariri na Uwajibikaji, na kwamba hawana uhakika kama kuna taasisi nyingine ya kisiasa iliyofanya hivyo.
“Tunapenda kutumia fursa hii kuwahakikishia wadau wote wa habari, wakiwemo waandishi, wahariri na wananchi, kuwa tutaendelea kuionesha imani hiyo kwa vitendo katika shughuli zetu zote za kisiasa,” alisema Mrema.
Post a Comment
Post a Comment