Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza DCP Ahmed Msangi amemtaja mtuhumiwa huyo kuwa ni Nyamisi Bahati (27) anayedaiwa kumuua mtoto wake aitwaye Sakimu Hassani baada ya kumtupa ziwa Victoria na kupelekea mtoto huyo kupoteza maisha, tukio analodaiwa kulifanya majira ya saa 1:00 usiku ya tarehe 13/06/ 2017.
Inadaiwa mtuhumiwa ambaye ni mama wa mtoto huyo alitoka nyumbani kwa mumewe na kwenda kuwasalimia wazazi wake akiwa na mtoto wake, lakini baadaye alitoka nje akiwa na mtoto kama anakwenda kumbembeleza ndipo baada ya muda kupita alirudi akiwa hana mtoto na kupelekea Mama yake mzazi wa binti huyo kumuuliza mtoto amemuweka wapi ndipo mtuhumiwa alionekana na mashaka huku akishindwa kuonyesha mahali mtoto alipo na baadaye akasema amemtupa kwenye Ziwa Victoria.
Kamanda Msangi amesema baada ya mtuhumiwa kusema hivyo, Bibi wa mtoto alipiga yowe akiomba msaada kwa watu ili waweze kuja kumuokoa mtoto na wananchi walipofika waliweza kutoa taarifa kituo cha Polisi na kuweza kufika eneo la tukio ambapo walishirikiana na wananchi na kufanya kazi ya kumtafuta majini na baadaye walifanikiwa kumpata ila alikuwa tayari ameshapoteza maisha.
Kamanda Msangi ameendelea kusema kuwa uchunguzi wa awali unaonyesha mtuhumiwa wa mauaji hayo anasumbuliwa na matatizo ya akili, japokuwa Polisi wapo katika upelelezi na mahojiano na mtuhumiwa pindi uchunguzi ukikamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.
Post a Comment
Post a Comment