Kufuatia tishio la kuwepo kwa programu mtumishi (software) yenye virusi aina ya WannaCry, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetoa onyo kwa watumiaji wa kompyuta kutofungua viambatanishi wasivyovijua kwenye barua pepe zao.
Aidha, taasisi zimetakiwa kutunza data nje ya mtandao ili kuepuka athari endapo kompyuta zitashambuliwa na virusi hivyo, sambamba na kuimarisha mifumo ya ulinzi dhidi ya virusi.
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, James Kilaba alibainisha kuenea kwa programu yenye virusi vinavyoathiri na kumzuia mtumiaji kufikia mafaili au mifumo, ama kwa kufungia mifumo ya screen au kuharibu faili kwenye kompyuta.
“Likitokea tatizo hilo, hackers (wadukuzi) wanadai kiasi fulani cha fedha ili kuweza kuzipata faili kwenye kompyuta. Kulipa hizo fedha hakukupi hakikisho la kupata mafaili yaliyoathirika, hivyo tunawashauri watumiaji na taasisi kutolipa fedha.
“Endapo mtumiaji au taasisi wanakumbwa na tatizo hilo basi watoe taarifa kwa Timu ya kitaifa ya dharura ya kompyuta (TZCERT),” alisema.
Kilaba alisema tishio la virusi WannaCry haliko kwenye kompyuta pekee bali pia kwenye simu za kisasa endapo utafungua kiambatanisho au link yenye virusi hivyo.
Kilaba alisema virusi WannaCry kinaharibu programu za kwenye kompyuta zilizopitwa na wakati au software zenye shida hususani Microsoft Server Message Block 1.0 (SMBv1) zilizotolewa mapema mwaka huu na Microsoft kama njia ya kuzuia mazingira magumu na watumiaji wa Microsoft wanaweza kuokoa kompyuta zao kwa kuweka njia za usalama.
Post a Comment
Post a Comment