KAMBI ya Rasmi ya Upinzani Bungeni imebainisha mambo zaidi ya 10 ambayo hairidhishwi nayo katika serikali ya awamu ya tano.
Kiongozi wa kambi hiyo,Freeman Mbowe, ndiye aliyataja mambo hayo wakati akiwasilisha hotuba yake bungeni juzi kuhusu makadirio ya bajeti ya serikali kwa mwaka ujao wa fedha.
Mbowe alisema mambo hayo ni pamoja na alichokiita uonevu wa viongozi na wabunge wa vyama vya upinzani akiwatolea mfano wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (chadema).
Mbowe aliwataja wabunge Peter Lijualikali aliyehukumiwa kifungo cha miezi sita jela badala ya faini lakini hukumu hiyo ikatenguliwa na Mahakama Kuu na Godbless Lema.
Lema alinyimwa dhamana licha ya kuwa na haki ya kupatiwa na kulazimika kuwekwa mahabusu gerezani kwa takribani miezi minne.
Mbowe alizungumzia pia kitendo cha Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu na yeye mwenyewe kukamatwa mara kwa mara na Jeshi la Polisi wakati wakitekeleza majukumu yao ya kisiasa.
Mbowe alitaja mambo mengine kuwa ni kupotea kwa baadhi ya watu katika mazingira ya kutatanisha na kutoa mfano wa msaidizi wake, Ben Saanane.
Aidha, Mbowe alisema, upinzani haufurahishwi na kutochunguzwa na kuchukuliwa hatua kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ambaye ana tuhuma za kutumia cheti cha kitaaluma cha mtu mwingine kujiunga na elimu ya juu.
Alisema mambo mengine wanayochukizwa nayo ni ukiukwaji wa demokrasia na utawala wa sheria kutokana serikali kuzuia mikutano ya vyama vya siasa na kupiga marufuku urushwaji wa moja kwa moja wa vikao vya Bunge.
Aidha, Mbowe alisema, kitendo cha polisi kuua majambazi badala ya kuwakamata na kuwachukulia hatua za kisheria ni kasoro nyingine.
Mbowe pia alidai kuna uonevu unaofanywa na vyombo vya dola dhidi ya wananchi wa visiwa vya Unguja na Pemba wanaounga mkono vyama vya upinzani hususan Chama cha Wananchi (CUF), na kuwekwa kando kwa mchakato wa katiba mpya licha ya kugharimu mabilioni ya shilingi.
Mbowe pia alisema hali ya uchumi wa nchi ni mbaya huku akiishauri serikali kufanyia kazi onyo lililotolewa kwa Tanzania na Shirika la Fedha Duniani (IMF) hivi karibuni ili kuiepusha nchi kuingia kwenye anguko la uchumi.
Mbowe ambaye ni Mbunge wa Hai, alitaka serikali ya awamu ya tano kutilia mkazo kilimo na mkakati wa kuinua uchumi vijijini na kusikitishwa na kupaa kwa Deni la Taifa.
Kambi rasmi ya upinzani pia haipendezwi na kasoro zilizopo katika mikataba ya kimataifa ikiwamo ya madini, changamoto ya ajira kwa vijana, kutozingatiwa kwa misingi ya sheria na haki za binadamu katika kushughulikia sakata la dawa za kulevya na utekelezaji wa kusuasua wa bajeti ya serikali kwa mwaka huu wa fedha.
FARU JOHN
Akichangia mjadala wa makadirio ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka ujao wa fedha juzi, Lema alisema ameshangaa kuona serikali inatumia fedha nyingi kupata ushahidi wa Faru John huku ikiacha kushughulikia kupotea kwa Saanane.
Mbunge huyo ambaye katika kuchangia kwake alilazimika kujibizana kwa kunukuu mistari ya kwenye Biblia na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tamisemi, George Simbachawene, alisema anatamani kuona wabunge wakienda jela walau kwa miezi minne tu ili wakirejea kutoka huko, watakuwa wameachana na uoga na kutunga sheria zitakazonufaisha kizazi kilichopo na kijacho.
Post a Comment
Post a Comment