MIAKA kadhaa iliyopita wakati serikali ya Tanzania ikitangaza kuhama kutoka mfumo wa analojia kwenda dijitali wengi waliingiwa hofu, na walikuwa wakilalamika wasijue kesho yao ingekuwaje.
Leo baada ya mfumo wa dijitali kufanikiwa katika kila eneo la maisha ya Watanzania, wengi wao wanafurahia maisha ya kidijitali na kwa hakika, wengi wameusahau kabisa mfumo wa analojia.
Huo ulikuwa ni ulimwengu wa kulalamika bila kujua nini kinakuja; kulalamika bila kuangalia faida lukuki za maendeleo yaletwayo na kukua kwa teknolojia na mifumo ya fedha ya kielektroniki.
Ni malalamiko hayo hayo yaliyokuwa yakisika hata miongoni mwa wapenda soka wa Tanzania wakati serikali ilipotangaza kuanzishwa kwa mchakato wa kuachana na matumizi ya tiketi za vishina viwanjani, ili kuhamia katika mfumo wa kadi za kielektroniki.
Sasa inafahamika kwamba asilimia kubwa ya waliokuwa wakilalamikia kuanza kwa matumizi ya mfumo wa tiketi za kielektroniki viwanjani, na hasa Uwanja wa Taifa na Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, ni waliokuwa wanuifaika wakubwa wa tiketi za vishina, nyingi zilizokuwa ni bandia.
Mwaka jana serikali kupitia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ilipokata shauri na kuamua kutumia kadi za kielektroniki, kazi hiyo ilikabidhiwa kwa Kampuni ya Selcom Tanzania.
Awali kazi ilionekana kama ngumu, lakini jaribio la kwanza lilizaa matunda mazuri kama ambavyo ripoti ya majaribio hayo katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam inavyoeleza: “Mfumo huu ulianza kutumika rasmi Oktoba Mosi, 2016 katika mechi ya Simba na Yanga iliyofanyika Uwanja wa Taifa.
“Mfumo umekuwa na mafanikio makubwa tangu uanzishwe, mashabiki wengi wa mpira wa miguu wanaufurahia kutokana na uwazi wake,” inasema ripoti hiyo iliyoandaliwa na Selcom na kupelekwa serikalini, TFF na klabu za soka zinazoshiriki Ligi Kuu ya Soka nchini (VPL).
“Kwa bahati nzuri miongoni mwa masuala yenye mafanikio makubwa katika mfumo huu wa tiketi za kielektroniki ni uwazi. Sasa, kwa mfano, tunaweza kujua, kwa hakika, kwamba mechi ya watani wa jadi, yaani Simba na Yanga ya Oktoba mwaka jana iliingiza mapato kiasi gani?
Mgawanyo wa mapato ulikuwaje? Na ni idadi gani ya mashabiki wa klabu hizo mbili na wapenda soka wengine waliolipa kuinga uwanjani?
“Ripoti ya Selcom inasema kuhusu mapato na watazamaji walioingia uwanjani siku hiyo ya Oktoba Mosi mwaka jana: “Mchanganuo wa mapato katika mechi ya Simba na Yanga iliyochezwa Oktoba 1, 2016 upo. Idadi ya mashabiki walioingia ni 44,291 ambao waliingiza kiasi cha Sh. 354,397,000 (milioni 354.3).
“Vilevile takwimu zinaonyesha mashabiki walioingia jukwaa la VIP B na C ni 2762, waliongia VIP A 498 na waliongia kwenye majukwaa mengine ya mzunguko walikua 41,031.”
“Katika kuhakikisha mashabiki wa soka hawapati taabu ya kununua tiketi kila wakati wa mchezo, Selcom ilianzisha utaratibu wa kusambaza kadi ambazo hutumika kuweka fedha na kuingilia uwanjani kwa kuigusisha kwenye mashine iliyowekwa getini.
“Hadi sasa imesambaza na kusajili kadi 168,000 ambazo zinaendelea kutumika kwa nyakati tofauti kuingilia kwenye mechi zinazofanyika Uwanja wa Taifa na Uwanja wa Uhuru. Zoezi la kusambaza kadi bado linaendelea kwa kasi kubwa na sasa watu wana uelewa zaidi wa matumizi ya kadi zao za Selcom.”
Maswali yamekuwa machache kutoka kwa washiriki wapya baada ya elimu endelevu inayotolewa kila wakati. Miongoni mwa faida za mfumo huu kwa kiasi kikubwa ni kumudu kudhibiti uvujaji wa mapato uliokuwapo awali, ambacho kilikua ni kilio cha muda mrefu cha klabu za soka zilizokuwa zikikosa mapato yaliyokuwa yakivuja sana.
Vilevile utaratibu wa kununua tiketi umerahisishwa. Huko nyuma mashabiki walipata taabu kununua tiketi hasa katika mechi kubwa.
Sasa mtu anaweza kununua tiketi yake na ya rafiki yake kwa Selcom Card kupitia simu ya mkononi, anachotakiwa kufanya ni kuongeza salio kwenye kadi yake kwa wakala yoyote wa Selcom kisha apige *150*50# na kuchagua namba 3 (Burudani/Michezo) kisha achague tiketi ya mechi.
Pia kwa kutumia hiyo hiyo Selcom Card watumiaji wanaweza kufanya miamala mingine mingi kama kununua LUKU, vocha, malipo ya maji, NHC na TRA, michango ya PPF, PSPF, kufanya malipo ya huduma kwenye vituo vya mafuta, supermarket, migahawa, maduka nk.
Utaratibu huu unasaidia kutunza kumbukumbu kwa kila mtu aliyenunua tiketi, takwimu pamoja na taarifa za makusanyo na mchanganuo wa mapato hutolewa kila mechi inapochezwa na kutumiwa wahusika wakiwamo klabu husika, TFF, Wizara, Bodi ya Ligi na vyama vya soka.
Kutokana na mfumo huu imewezekana kudhibiti watu wanaoingia uwanjani kwa njia ya wizi kwa asilimia 99.99. Hata hivyo, bado kuna wachache ambao wanahitaji elimu ya kutosha kuhusiana na utaratibu wa kadi moja mtu mmoja, ndiyo maana Selcom inaendelea kutoa elimu ya kutosha kupitia kwa mawakala wake kwenda kwa watumiaji wa mfumo, ili waweze kuelewa kwa kina.
Aidha, ili mambo yawe mazuri zaidi, pana haja ya kuwa na ushirikiano mkubwa na wa karibu wa kutoa elimu kati ya TFF, sekta mbalimbali za Serikali na wadau wote katika kuhakikisha kuwa elimu inawafikia walengwa na kwa wakati.
Wadau kadhaa wa soka wamejitokeza kuzungumzia mfumo huu. Hilal Said ni Meneja wa Klabu ya soka Coastal Union ya Tanga inayoshiriki ligi daraja la kwanza. Anasema mfumo huo mpya utawasaidia kudhibiti mapato ya mlangoni.
"Mechi nyingi tulizocheza katika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam kati ya Simba au Yanga tulipunjwa mgawo. Utakuta Uwanja umefurika lakini yakija mahesabu mnapata kiasi kidogo. Huwezi kulalamika kwa sababu tiketi za karatasi huwezi kujua idadi yake, lakini hizi za kieletroniki mahesabu yapo wazi," anaeleza Hilal.
Kwa upande wake mshabiki wa soka ambaye pia aliwahi kuzichezea klabu za African Sports na Coastal Union za Tanga kabla ya kujiunga na Simba ya jijini katika miaka ya 1980 na mapema 1990, Razak Yussuf 'Careca'
anazungumzia suala la usalama ndani ya uwanja.
"Mimi siwezi kusema ni shabiki wa timu gani, lakini mara nyingi Simba na Yanga zinapocheza nakwenda Dar es Salaam kushuhudia, lakini kinachoniudhi ni fujo uwanja unafurika sana bila utaratibu.
"Nashukuru mara ya mwisho wakati tulipoingia uwanjani kwa tiketi za kielektroniki hali ilikuwa nzuri, kwa sababu uzuri wa kadi hizi idadi ya uwezo wa uwanja ikifikia haingii mtu, kinyume na zamani watu walikua wanaingia tu," anaeleza Careca.
Vyombo vya ulinzi na usalama vinaombwa kusaidia kwa kina katika kuhakikisha kuna amani na utulivu wakati wa zoezi zima la kuingia uwanjani.
Kuwapo kwa utaratibu wa kupanga foleni wakati wa kuingia uwanjani na viwepo vizuizi ambavyo vitawaongoza mashabiki katika kuingia uwanjani kwa ustaarabu na kwa kupeana nafasi.
Akizungumzia namna walivyofanikisha jaribio la awali Meneja Miradi wa Selcom Gallus Runyeta anasema uuzaji wa kadi ulichukua wiki moja hiyo ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa watumiaji na kusimamia kila kituo ili kusiwapo na udanganyifu.
Hata hivyo, mafanikio hayakosi changamoto, yapo masuala mbalimbali Selcom imejifunza kutoka kwenye changamoto zilijitokeza wakati wa mashabiki kuingia uwanjani, kuhakiki tiketi na imejipanga vyema kwa michezo inaoyofuata.
Selcom imekuwa mstari wa mbele katika kuchukua ushauri wa maboresho ya mfumo kutokana na matumizi ya kila siku ya mfumo wa kielektroniki katika Uwanja wa Taifa na Uwanja wa Uhuru ili kuongeza tija katika kufanikisha ufanisi wa mfumo kwa asilimia 99.99.
Kwa ajili hiyo Selcom imefanya maboresho yafuatayo; imepanua wigo mkubwa kwa kupunguza muda wa mashine wakati kadi ya kielektroniki inapogusishwa kwenye mashine na kufungua kutoka sekunde mbili za mwanzoni mpaka nusu sekunde ili kutoa nafasi kwa watu wengi zaidi kuingia uwanjani katika muda mfupi.
Iliamua kuagiza kwa gharama zake, kufanya maandalizi na kusimika kadi tofauti ambazo zinaongeza tija katika kufanya uhakiki wa tiketi za kielektroniki kwa haraka na kwa ufanisi wa hali ya juu.
Imeweka timu ya wataalamu wa kutosha uwanjani ambao wanatoa ufumbuzi kwa changamoto zozote za kiufundi zinazojitokeza uwanjani.
“Timu hii ina simu maalumu kwa ajili ya kujibu na kurekebisha marekebisho madogo madogo yote, tumepanua wigo wa mawakala zaidi ya 5000 Tanzania nzima na kuwapa uwezo wa kuuza tiketi moja kwa moja kwenye kadi za mashabiki kwa uharaka zaidi na kwa usalama wa kutosha.
“Tumeweka punguzo kubwa la bei ya kadi hadi kufikia Sh. 1,000 kwa kadi, zoezi hili limejumuisha elimu kwa mashabiki kwani kadi hii huweza kutumika kila mara mtu aingiapo uwanjani,” anasema Runyeta.
Selcom Tanzania haikuishia hapo bali katika kila mechi za soka huweka matangazo ya kutosha uwanjani ili mashabiki waweza kujisajili na kununua wenyewe tiketi kwa urahisi, inaelezwa matokeo yamekuwa mazuri kwani imeonekana uelewa ni mpana kwa sasa.
Kama hiyo haitoshi, Selcom Tanzania imeweka utaratibu wa kutuma ujumbe mfupi kabla ya mechi ili kufanikisha mawasiliano ya mechi husika na kwa wakati ili kama kuna tatizo la kimfumo lipate ufumbuzi wa haraka kuepusha malalamiko kutoka kwa mashabiki.
Februari 25 mwaka huu katika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam kutakuwa na mechi kati ya Simba na Yanga, mashabiki wanatakiwa kuweka Selcom Card zao tayari.
Pia wanaweza kufuatilia taarifa mbalimbali za mechi hiyo kutoka katika mtandao na tovuti mbalimbali za wadau wa huduma hii ili wajionee.
Post a Comment
Post a Comment