Kiwango cha joto kimeshuka hadi nyuzi 23 chini ya sifuri katika baadhi ya maeneo ya Ulaya. Hali hii imesababisha maafa na hata watu kufa. maisha ya wakimbizi na watu wasiokuwa na mahala pa kuishi yako hatarini
Bara zima la Ulaya linatetemeka kwa baridi kali kutokana na kushuka kwa viwango vya nyuzi joto katika msimu huu wa baridi. Watu kadhaa wameripotiwa kufa kutokana na baridi kali. Hali hii ya baridi ya kupindukia imesababisha pia mtafaruku katika utaratibu wa usafiri na wakati huohuo wakimbizi waliokwama katika kisiwa cha Chios nchini Ugiriki wanakabiliwa na hali mbaya.
Hali hii mbaya ya baridi kali inawakumba pia wakimbizi walioko katika kisiwa cha Lesbos ambapo inaripotiwa kuwa hawana maji wala umeme. Takriban watu elfu 15 wanasubiri kurudishwa nchini Uturuki kufuatia makubaliano yaliyofikiwa baina ya Umoja wa Ulaya na serikalri ya Ankara.
Huko Ujerumani dereva mmoja ambaye anajishughulisha na kuwasafirisha watu kinyume cha sheria aliwatelekeza abiria wake 19 ndani ya gari alilokuwa akiwasafirishia. Dereva huyo aliliacha gari hilo katika maegesho na kuamua kutoweka bila kuwajulisha abiria wake hao katika jimbo la Bavaria na wakati huo kulikuwa na baridi ya kiwango kilichoshuka zaidi cha nyuzi 20 chini ya sifuri.
Polisi wameeleza kuwa watu hao 14 na watoto watano walikuwa wamemlipa dereva huyo kiasi cha Euro 500 hadi 800 na kwamba huenda dereva huyo aliamua kuwaacha baada ya kutambua kuwa gari lake lina matatizo ya kimitambo.
Hali ya baridi kali na kuanguka kwa theluji katika maeneo mbalimbali katika siku za hivi karibuni imesabaisha madhila katika maeneo mengi barani Ulaya.
Kwingineko takriban watu 9 wamekufa nchini Poland watatu katika Jamuhuri ya Czech na wawili nchini Holand. Taarifa zilizoandikwa na Mtandao wa DW zinaeleza kuwa wengi wa watu wanaokumbwa na umauti ni wale ambao hawana mahala pa kuishi. Polisi nchini Poland wamesema kuwa wanatarajia idadi ya vifo kuongezeka.
Nchini Ufaransa abiria wanne raia wa Ureno walikufa baada ya basi walilokuwa wakisafiria kuteleza na kuacha njia katika eneo la mji wa Lyon taarifa kutoka wizara ya mambo ya ndani ya Ufaransa zinaeeleza kuwa chanzo cha ajali hiyo huenda kilitokana na mtelezo katika barabara uliosababishwa na barafu inayoteleza.
Ujerumani, Italia, Ugiriki, Poland na Uturuki ni miongoni mwa nchi ambazo zinakabiliwa na kumwagika kwa theluji nyingi na kushuka kwa viwango vya joto huku Ujerumani ikijiandaa kwa hali mbaya ya hewa kutokana na dhoruba inayotazamiwa kutokea maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo.
Wataalamu wa hali ya hewa nchini Ujerumani wametahadharisha juu ya hatari za barafu nyeusi ambayo inateleza mno.
Post a Comment
Post a Comment