MAKAMU WA RAIS AAGIZA VIONGOZI WANAOIKWAMISHA SERIKALI WAKAMATWE

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan ameagiza vyombo vya dola nchini kuwakamata bila kuwaonea huruma viongozi watakaobainika kujihusisha au kuhujumu kazi ya kupambana na uvuvi haramu nchini.

Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan ametoa agizo hilo wakati akishiriki katika zoezi la uchomaji wa zana haramu za uvuvi 5,662 kwenye eneo la Buhongwa wilayani Nyamagana mkoani Mwanza zilizokamatwa katika Ziwa Victoria.

Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amesema kumekuwa na tabia ya baadhi ya viongozi kushiriki katika shughuli za uvuvi haramu hivyo inabidi wachukuliwe hatua ili kukomesha kabisa tatizo la uvuvi haramu katika Ziwa Victoria na maeneo mengine nchini.

Ameeleza kuwa uvuvi haramu katika Ziwa Victoria umekuwa ni tatizo sugu na hali ambayo imesababisha kupungua kwa samaki na mapato kwa Serikali ambayo ni muhimu kwa ajili ya shughuli maendeleo.

Amesema licha ya uvuvi haramu kupunguza mapato ya Serikali kutoka kwenye viwanda hali ya ajira nayo sio nzuri zilizokuwa zinatoka kwenye viwanda ambazo zimepungua kwa asilimi 49.

Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amepongeza kazi kubwa iliyofanyika ya ukamataji wa zana haramu za uvuvi katika Ziwa Victoria na amewahakikishia viongozi wa mkoa wa Mwanza kuwa Serikali ipo pamoja nao katika kazi hiyo.

“Serikali yenu itaendelea kushirikiana nayi katika kuhakikisha kuwa rasilimali za uvuvi katika Ziwa Victoria zinaendelea kuwepo kwa kuendelea kutoa fedha na vitendea kazi ili kuongeza ufanisi katika utendaji wa kazi kwa lengo la kuhifadhi ziwa Victoria” Amesisitiza Makamu wa Rais.

Kwa upande wake, Mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongela amesema oparesheni za uvuvi haramu katika Ziwa Victoria zitaendelea kuimarishwa ipasavyo mkoani Mwanza mpaka vitendo hivyo vikomeshwa.

Amesema mkoa wa Mwanza ulikuwa na viwanda Sita vya kuchakata samaki lakini kutokana na kupungua kwa samaki katika Ziwa Victoria ni viwanda Vinne tu mpaka sasa ndio vinafanya kazi hali ambayo imepunguza kwa kiasi kikubwa mapato kwa Serikali na ajira kwa vijana mkoani huo.

Mkuu huyo wa Mkoa wa Mwanza John Mongela ameeleza kuwa kutokana na viwanda hivyo kusitisha shughuli za uzalishaji zaidi ya watu mamia ya watu wamekosa ajira.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia kwenye shughuli za mazingira ambapo nyavu zilizotumika kwenye uvuvi haramu zimeteketezwa katika dampo la Buhongwa, wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akishiriki kuchoma nyavu za uvuvi haramu kwenye dampo la Buhongwa, wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)

Related Posts

Post a Comment