Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu amesema kuwa watakwenda mahakamani kupinga maamuzi ya kusimamishwa kwa wabunge wa CHADEMA, Esther Bulaya (Bunda) na Halima Mdee (Kawe) baada ya kupewa adhabu hiyo mwanzoni mwa wiki walipopatikana na hatia ya kudharau Mamlaka ya Spika wa Bunge.
Lissu amesema kuwa atakutana na wabunge hao waliosimamishwa na kuandaa hoja watakazopeleka Mahakama Kuu na kwamba uamuzi aliochukua Spika wa kuwafungia wabunge hao wa kutohudhuria vikao vya Bunge kwa miezi kumi ni makosa makubwa.
Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai.
“Tunataka Mahakama ituambie kwenye ‘Judicial review’ je, Bunge linaweza kufuta ubunge wa Mbunge wake, kama wanavyotafsiri hawa akina Ndugai? Je, Bunge linaweza likatoa adhabu hata nje ya adhabu iliyopo kwenye kanuni? Je, Bunge lina uwezo wa kumuadhibu Mbunge bila kumpa fursa ya kujitetea kwenye Kamati na Bunge lenyewe?
Tutaomba Mahakama Kuu itupe tafsiri. Kwa vyovyote vile utaratibu huu hatutakubaliana nao. Tukienda hivi, hawa CCM wa Bungeni kuna siku wataamua Mbunge asiingie Bungeni kwa miaka mitano halafu wanasema Bunge lina mamlaka lisiingiliwe. Bunge haina mamlaka hayo.
Kuna kanuni za kutoa adhabu kwa Mbunge yeyote anayefanya kosa. Adhabu ya kumfungia Mbunge kwa miezi 10 haipo kwenye Kanuni za Bunge la Tanzania. Lakini kumekuwa na tabia na utamaduni, sasa inapofika wabunge wa upinzani wanapewa adhabu kubwa kubwa ambazo zipo nje kabisa ya utaratibu wa kanuni zilizopo,” alisema Lissu.
Amesema kuwa Sheria na kanuni za Bunge zinasema adhabu ya Mbunge ni kumfungia vikao 20 kwa maana ya siku na kwamba adhabu nyinginezo haiwezi ikawa kifungo cha siku 100 au miezi kumi. Pia alisema kuwa tafsiri nyengine ya kanuni hizo si kumzuia Mbunge kuhudhuria vikao 20, bali inaweza ikawa kumnyima Mbunge huyo mshahara wake, kuzuia bima yake ya afya na kumfutia posho ya jimbo.
Post a Comment
Post a Comment