BUNGE HUENDA LIKAPIGA KURA YA KUTOKUWA NA IMANI NA RAIS MAGUFULI


Chama cha ACT-Wazalendo kimesema kuwa kitawasilisha bungeni hoja ya kutokuwa na imani na Rais Magufuli kufuatia sakata la njaa ambapo baadhi ya wananchi wanakufa kwa kukosa chakula.

Hayo yalisemwa na Mbunge wa Kigoma Mjini na kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe alipokuwa akimnadi mgombea udiwani katika Kata ya Kijichi.

Zitto Kabwe alisema kuwa Rais Magufuli atakuwa ndiye rais wa kwanza wa Tanzania kupigiwa kura ya kutokuwa na imani kwa kuacha wananchi wafe njaa.

Kwa mujibu wa katiba ibara ya 46 (a), wabunge wataweza kujadili kuhusu kura ya kutokuwa na imani na rais endapo asilimia 20 ya wabunge wataiunga mkono hoja hiyo, alisema Zitto. Alisisitiza kuwa, endapo wabunge wa upinzani wataungana, basi Rais Magufuli atakuwa wa kwanza kupigiwa kura ya kutokuwa na imani.

Aidha, Zitto Kabwe alimtaka Rais Magufuli kuacha kurusha lawama kwa wanasiasa na vyombo vya habari kwa madai kuwa vinalifanya jambo la njaa kuwa la kisiasa. Sisi ACT-Wazalendo tunamtaka rais ashughulikie suala hili na si kweli kuwa kila mwenye mawazo tofauti na ya serikali basi amehongwa, alisema Zitto.

Kiongozi huyo alisema kuwa chama anachokiongoza hakitanyamaza kamwe mambo yanapokuwa hayaendi sawa huku akiwataka wananchi kuzungumza ukweli bila woga kuhusu hali ya njaa nchini.

Rais Magufuli mara kadhaa amekuwa akinukuliwa akisema kuwa hakutakuwapo na chakula cha bure kwa watu ambao hawana vyakula. Akiwa mkoani Simiyu alisema kuwa serikali inajikita kufanya mambo makubwa hivyo masuala kama chakula ni ya kushughuliwa na wananchi na si serikali irudi tena kuja kugawa chakula.

Related Posts

Post a Comment