Njombe
Wakulima wa Parachichi mkoani Njombe wameamua kuanzisha chama cha kuweka na kukopa (Saccos) kwa ajili ya kusaidia wakulima wadogo ambao wamekosa vigezo vya kukopesheka kwenye benki nyingine kutokana na masharti magumu.
Hayo yamesemwa na mkurugenzi wa asasi ya wakulima wa Parachichi nyanda za juu kusini (NSHIDA) Frank Msigwa kwenye mkutano mkuu wa wakulima wa zao hilo uliofanyika mkoani Njombe.
Amesema sababu ya kuanzisha Saccos hiyo ni kuwa asilimia 95 ya wakulima wa Parachichi mkoani humo hawana sifa ya kukopesheka kwenye mabenki.
Amesema wamefanya juhudi za kuunganisha wakulima na mabenki lakini ni asilimia tano pekee ndiyo yamefanikiwa kupata mikopo na haswa ni wakulima wakubwa ambao wana uwezo.
"Sasa tumekuja na hili wazo sisi kama NSHIDA tukiwa na Saccos hii tunamkopesha mkulima hata mwenye mti mmoja wa Parachichi kwa masharti nafuu kwakuwa ni benki yetu sisi wenyewe na tunafahamiana" amesema Msigwa.
Amesema wakulima wanastahili kukopesheka kwasababu wana uwezo wa kulipa kwakuwa masoko ya uhakika yapo.
Amesema Njombe kuna zaidi ya kampuni kumi na tano yamefika kwa ajili ya kununua Parachichi hivyo mkulima akiwezeshwa kwenye miundo mbinu ya maji, pembejeo na dawa atazalisha Parachichi iliyo bora na kuuzika kirahisi.
Ameiomba wizara ya kilimo kuwaongezea nguvu ili wakulima waweze kupata mitaji ya kuendesha shughuli za kilimo.
Afisa ushirika wa tume ya maendeleo ya ushirika Tanzania Idd Chamshama amesema serikali inatambua kuwa ushirika ni nyenzo muhimu ya kuwezesha wananchi kiuchumi hasa wakulima wadogo.
Amesema jukumu la serikali ni kuendelea kuhamasisha wananchi kuanzisha vyama vya ushirika kwa malengo ya kujikomboa na umasikini na kuboresha maisha yao.
"Kwahiyo serikali kupitia sera ya maendeleo ya ushirika inahimiza uanzishwaji wa vyama vya ushirika ambavyo ni imara na endelevu vitakavyokidhi matarajio ya wanachama" amesema Chamshama.
Diwani wa kata ya Njombe Mjini Alatanga Nyagawa amesema ili wakulima wa Parachichi mkoani Njombe waweze kukua kiuchumi na kutatua changamoto zinazowakabili ni lazima waungane.
"Fursa tulizonazo kwenye Parachichi ni lazima tuitumie kwa kutafuta masoko ya uhakika ili wakulima wetu wakue kiuchumi" amesema Nyagawa.
Baadhi ya wakulima wa Parachichi mkoani Njombe akiwemo Tumaini Mhoka amesema kuanzishwa kwa chama hicho kitawasaidia wakulima kuongeza uzalishaji wa zao hilo na kuwa na masoko ya uhakika.
"Ukienda benki unaambiwa ulete dhamana sasa wewe ni mkulima ndiyo unaanza na wanataka hati sasa wengi wetu hatuna na wakati mwingine ukifanikiwa kuchukua mkpo mwezi unaofuata unaambiwa uanze kulipa wakati unategemea ulime uvune kisha ndiyo uuze na kulipa madeni" amesema Mhoka.
Post a Comment
Post a Comment