News
Njombe
Katika kuadhimisha miaka 47 ya kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi,Jumuiya ya Umoja wa wanawake wa Chama hicho wilayani Njombe umetumia maadhimisho hayo katika kupanda miti ya matunda ya Parachichi kwa kuanzia katika shule ya sekondari ya wasichana ya Manyunyu iliyopo Lupembe wilayani humo kwa lengo la kuunga mkono juhudi za Rais Samia pamoja na serikali ya mkoa wa Njombe kwenye vita dhidi ya udumavu na utapimlo ili kupata matunda shuleni pamoja na kutunza mazingira.
Katibu wa Chama hicho wilaya ya Njombe Sure Mwasanguti ameongoza zoezi hilo ambapo amesema walichofanya UWT ni kuenzi kazi anazofanya Rais kwasababu hata siku yake ya kuzaliwa aliweza kupanda miti.
"Mmemuunga mkono Dkt.Samia Suluhu Hassan na ninyi mmepanda Parachichi ambapo watoto wetu watakula chakula bora kwa lengo la kuondoa udumavu kwenye mkoa wetu wa Njombe hapa UWT mmeweka alama"amesema Mwasanguti
Kwa Upande wake mwenyekiti wa UWT Betreace Malekela amesema mambo makubwa yamefanywa na serikali ya awamu ya sita hivyo kutimiza miaka 47 ya chama chao kinaonyesha ukubwa walio nao huku akitoa wito kwa wanachama kuendelea kushikamana.
"Niwaombe sasa ndugu zangu tuendelee kushirikiana na kushikamana kwa pamoja na kuto kudanganyika na hiyo ndio dhamira ya Chama cha Mapinduzi ili tuendelee kufika mbali"amesema Betreace
Nao baadhi ya washiriki wa hafla hiyo wakiwemo madiwani wamepongeza uongozi wa CCM wilaya pamoja na Jumuiya kwa kufikiria kwenda kupanda miti kwa ajili ya matunda ili yaweze kuliwa na wanafunzi kwa lengo la kuendelea kutokomeza udumavu.
Post a Comment
Post a Comment