Wanahabari wanne wa vyombo mbalimbali vya habari wilaya ya Kahama wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kujipatia Sh1milioni kutoka kwa mganga wa jadi baada ya kujifanya maofisa Usalama wa Taifa.
Akizungumza leo Januari 10, 2018 Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga, Simon Haule amewataja waandishi hao na vyombo vyao katika mabano kuwa ni Paul Kayanda (gazeti la Uhuru), Shaban Njia (Nipashe), Simon Dionis (Radio Kwizera) na Raymond Mihayo wa gazeti la Habari leo, huku mmoja akikimbia.
Amesema watuhumiwa hao walitenda kosa hilo jana Januari 9 saa 7 mchana katika kitongoji cha Ng’wande kijiji cha Bani wilayani Kahama baada ya kumtishia mganga huyo, Jane Mbeshi (46) kuwa wao ni maofisa usalama kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Kigoma, Kagera, Shinyanga na Kahama.
Amebainisha kuwa baada ya kujitambulisha, walimtaka mganga huyo kuwapa kiasi cha Sh2 milioni ili wasimtie mbaroni kwa kosa la kupiga ramli chonganishi.
“Januari 6 watuhumiwa walipokea Sh1 milioni kutoka kwa mganga huyo kwa makubaliano kuwa kiasi kingine kilichosalia wangepewa siku nyingine,” amesema Haule na kuongeza,
“Baada ya kupokea taarifa hizo polisi waliweka mtego na kufanikiwa kuwatia mbaroni watuhumiwa watatu kati ya watano waliofika nyumbani kwa mganga huyo kupokea kiasi cha fedha kilichosalia.”
Amesema waliokamatwa kwenye eneo la tukio ni Kayanda, Njia na Dionis huku Mihayo akijisalimisha mwenyewe polisi jana, kwamba mtuhumiwa wa tano, George Maziku anaendelea kusakwa na polisi.
Post a Comment
Post a Comment