Akizungumza na wananchi moja kwa moja kutoka Ikulu, Rais Kenyatta aliyekuwa ameambatana na Makamu wa Rais, William Ruto amewasihi wa Kenya kulinda amani yao bila kujali itakadi zao za vyama, dini au rangi kwani jirani yao ataendelea kuwepo hata kama wanatofauti kivyovyote.
Akizungumzia maamuzi ya mahakama, Rais Kenyatta alisema kuwa hakubaliani nayo lakini anaheshimu sheria na kwamba yupo tayari kurudi kwa wananchi kuomba kura katika uchaguzi utakaofanyika ndani ya siku 60 zijazo.
Rais Kenyatta alisema kwamba hayupo katika ugomvi na vyama vya upinzani na kuvitaka kutoendesha siasa za chuki bali wapinge hoja kwa hoja.
“Hatuko kwenye vita na ndugu zetu wa upinzani. Tuko tayari kurudi kwa debe, kuongea na Wakenya, kuwaambia yale tunataka na yale tunataka kutenda. Watu wachache, watu sita, hawawezi kubadilisha nia ya Wakenya milioni 40. Wakenya ndio wataamua, na hivyo ndivyo demokrasia ilivyo.”
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Tume ya Uchuguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC) amesema kuwa watu wote waliohusika katika kuvuruga uchaguzi ni lazima washughulikiwe.
Wafula Chebukat amemualika Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kufanya uchunguzi na kuwafungulia mashtaka watu wowote ambao walihusika kuvuruga uchaguzi.
Aidha, ameitaka Mahakama ya Juu iliyobatilisha uchaguzi huo, kuta haraka uamuzi wa kina kuhusu uchaguzi ili tume iweze kujiandaa na uchaguzi ujao.
Post a Comment
Post a Comment