Waziri wa Ulinzi, Dkt. Hussein Mwinyi amesema vijana ambao watakaidi wito wa kuhudhuria mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mujibu wa Sheria watakuwa wamekaidi amri halali na majina yao yatapelekwa mamlaka za ajira kwa ajili ya hatua dhidi yao.
Kauli hiyo ameitoa wakati JKT ikiendelea na mchakato wa kufufua kambi tano nchini ili kufanikisha uwezeshaji wa vijana wanaomaliza Elimu ya juu ya Sekondari kujiunga na Jeshi hilo kwa kujitolea na kwa mujibu wa Sheria.
Awali, ilikuwa lazima kwa wahitimu wa Elimu ya juu ya sekondari na vyuo kujiunga na mafunzo ya mwaka mmoja wa JKT kabla ya kuendelea na masomo au kuanza ajira, na baadaye muda ukapunguzwa. Lakini sasa, wanaojiunga ni wale wanaoitwa tu.
Waziri Mwinyi alisema uchaguzi wa vijana wanaotakiwa kujiunga na mafunzo hayo unafanyika bila kutumia kigezo chochote zaidi ya kuwa mhitimu wa kidato cha sita.
“Yeyote ambaye jina lake linakuwa kwenye orodha ya wanaotakiwa kuhudhuria mafunzo, ni lazima akahudhurie na asipoenda anakuwa amekiuka amri halali. Majina ya walioteuliwa yalionesha waliohudhuria na waliokaidi tunayapeleka katika mamlaka za ajira,” alisema Dkt. Mwinyi.
Alisema orodha ya vijana ambao wanatakiwa kuhudhuria mafunzo hutolewa kwa awamu ili wote waweze kupata fursa ya kuhudhuria, lakini wakati mwingine hufikia wakati muda wa kujiunga na vyuo ukiwa umeshafika.
“Wale ambao wanakuwa wamechelewa kupata mafunzo kwa sababu muda wa vyuo kufunguliwa unakuwa umefika, hawatachukuliwa hatua na wanatambulika,” alisema Dkt. Mwinyi.
Hivi karibuni wakati wa hafla ya kufunga mafunzo ya JKT kwa vijana wa kujitolea katika kambi ya 838 KJ Maramba wilayani Mkinga, Brigedia Jenerali John Mbungo alisema jeshi hilo linakusudia kufufua kambi tano.
Alizitaja kambi hizo kuwa ni 826 Mpwapwa mkoani Dodoma, 845 Itaka (Songwe), 846 na 847 zilizoko Rukwa na 836 na 839 Makuyuni (Arusha) ambayo imeshaanza kupokea vijana ambao wanaendelea na mafunzo.
Alisema huo ni utekelezaji wa azma ya serikali ya kuwezesha vijana wenye sifa za kujiunga mafunzo ya JKT kwa kujitolea na wahitimu wa kidato cha sita kuhudhuria mafunzo hayo.
HT @ MWANANCHI
Post a Comment
Post a Comment