NI wingu zito, ndivyo unavyoweza kusema baada ya maombi ya Kampuni ya Kufua Umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) kukwama, huku wakilazimika kuzima rasmi mitambo yao ya uzalishaji umeme.
Hatua hiyo imekuja baada ya kukwama kwa maombi ya kuongezewa muda wa miezi 55 ya leseni yake ya uzalishaji umeme kutokana na kusubiri uamuzi wa Ikulu.
Hali hiyo inajitokeza wakati mmiliki wa Kampuni ya Pan Afrika Power (PAP), Harbinder Singh Sethi na Mkurugenzi wa Kampuni ya VIP Engineering, James Rugemalira wakiwa tayari wamefikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya uhujumu uchumi, kutakatisha fedha na kuisababishia hasara Serikali.
Habari za uhakika zilizolifikia gazeti hili jana zilisema mitambo hiyo kwa sasa haizalishi umeme. MTANZANIA lilitembelea mitambo hiyo iliyoko Tegeta na kukuta wafanyakazi wachache ambao walikiri mitambo hiyo kutofanya kazi.
“Mitambo ilizimwa tangu siku ile walipomkamata Sethi,” alisema mmoja wa wafanyakazi wa kampuni hiyo ambaye hakuwa tayari kutajwa jina lake gazetini.
Pamoja na hatua hiyo inaelezwa kuwa kuna hatari ta kuitaifishwa kwa mitambo hiyo hasa baada ya Serikali kuweka ngumu katika utoaji wa leseni mpya ya biashara ya kuzalisha umeme kwa kampuni hiyo.
Licha ya hali hiyo leseni ya kampuni hiyo ilimalizika muda wake Julai 15, mwaka huu ambapo hadi sasa uamuzi wa kuitafisha mitambo hiyo kurudi kuwa mali za Tanesco ama laa ukisubiri uamuzi wa Ikulu.
Kwa sababu hiyo, kama Serikali itaendelea na msimamo wake dhidi ya IPTL ndiyo utakuwa mwisho wa miaka 23 ya IPTL. Kampuni hiyo ya IPTL iliingia chini tangu mwaka 1994 na kila mwezi imekuwa ikilipwa Sh. bilioni 5.943 na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) ikiwa ni gharama za uwekezaji mbali na gharama za umeme inaoliuzia shirika hilo.
Novemba 2014, baada ya Bunge kujadili Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu akaunti ya Tegeta Escrow, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), ilitoa maazimio manane ikiwa ni pamoja na kuangalia uwezekano wa kuichukua mitambo ya IPTL na kuimilikisha kwa Tanesco.
Siku chache baada ya Bunge kupitisha uamuzi huo ambao ulifanyiwa kazi kwa haraka kwa Profesa Sospeter Muhongo kujiuzulu nafasi yake.
Wengine ni Profesa Anna Tibaijuka ambaye pia alijiuzulu nafasi ya Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Jaji Frederick Werema aliyejiuzulu nafasi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Eliachim Maswi aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini alisimamishwa kazi pamoja na wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Tanesco waliotakiwa kuwajibishwa, kukaa pembeni baada ya muda wa bodi yao kwisha na ikaundwa nyingine.
Naye Spika wa Bunge wakati huo, Anne Makinda alitangaza kuwa wazi nafasi za wenyeviti wa kamati za Bunge ambao ni William Ngeleja, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala, Andrew Chenge aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti na Victor Mwambalaswa aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini.
Azimio jingine lililotaka Harbinder Singh Seth ambaye ni Mwenyekiti wa PAP kufikishwa mahakamani, lilitekelezwa hivi karibuni ambako yeye na mwenzake James Rugemalira wa VIP Engineering, walifikishwa mahakamani na kusomewa mashitaka 12 yakiwamo ya uhujumu uchumi na kutakatisha fedha.
Baadhi ya maazimio ambayo yalikuwa hayajafanyiwa kazi ni lile la pili lilolotaka Serikali iangalie uwezekano wa kuichukua mitambo ya IPTL na kuimilikisha kwa TANESCO.
Mei 11, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, wakati wa maswali ya papo kwa papo bungeni, alimuhoji Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuhusu kutokutekelezwa maazimio hayo ya Bunge kuhusu Escrow.
Akijibu swali hilo, Majaliwa alimuhakikishia Mbowe kuwa Serikali inaheshimu muhimili wa Bunge na kuthamini uamuzi wake. Alisema kunahitajika uchunguzi wa kina na yapo mambo ambayo yana umuhimu wa kufikishwa bungeni hivyo uchunguzi wa Serikali utakapokamilika yatawasilishwa bungeni.
Kwa sababu hiyo, inawezekana kuisha leseni hiyo ya IPTL sasa, kukachukuliwa kama moja ya njia ya kutekeleza azimio la lipi la Bunge.
Pia Juni 20 mwaka huu, akiwa ziarani mkoani Pwani, Rais John Magufuli, alisema serikali itaendelea kuchukua hatua dhidi ya watu wanaolihujumu Taifa ikiwamo kujihusisha na vitendo vya wizi na rushwa na haitakatishwa tamaa na watu wanaolalamika na kubeza juhudi hizo.
“Stiegler’s Gorge, mradi ambao ulifanyiwa utafiti tangu enzi ya Mwalimu Nyerere tukautelekeza. Nataka tujenge bwawa litakalozalisha umeme utakaotosheleza katika nchi yetu, nchi ya viwanda ili Watanzania wasilalamikie tena suala la umeme, nataka tuachane na umeme wa matapeli wanaokuja hapa wanawekeza kwa lengo la kutuibia.”
“Mimi nachukia wezi na kwa kweli wezi watakoma tu, awe mwizi wa Tanzania, awe mwizi wa Ulaya, awe anatoka magharibi, mashariki, kaskazini au kusini, mwizi ni mwizi tu,” alisema Rais Magufuli.
IPTL imekuwa ikilalamikiwa kuwa ni miongoni mwa miradi inayoiumiza Tanesco, hivyo kauli hiyo ya mkuu wa nchi inaweza kuwa siyo ishara njema kwa kampuni hiyo.
Chanzo: MTANZANIA
Post a Comment
Post a Comment