Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli Ijumaa ya Julai 07,2017 amekutana na wazee wasiojiweza wa Wilaya ya Chato na kutoa misaada mbalimbali ya vyakula kwa lengo la kuwapunguzia changamoto zinazowakabili.
Mama Janeth Magufuli amekabidhi msaada huo kwa wazee zaidi ya 400 kutoka kata 23 za Wilaya ya Chato mkoani Geita.
Akizungumza wakati wa utoaji wa msaada huo kwa wazee hao wa Chato Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli ameitaka jamii,watu binafsi,wadau wa maendeleo na taasisi mbalimbali kushirikiana kwa pamoja katika kuwasaidia wazee hapa nchini.
Mama Janeth amezitaja baadhi ya changamoto zinazowakabili wazee hao kuwa ni pamoja na vyakula,madawa na hata upendo na kuthaminiwa.
“Tunawaomba jamani mnaokaa na wazee muoneshe upendo,muwasaidie pale wanapohitaji msaada,kama wewe una nguvu basi msaidie hata kuchota maji na kukata kuni kwani hizo ndo Baraka zenyewe”
Kwa upande wao wazee hao wamemshukuru mke huyo wa Rais kwa moyo wake wa kujitolea hususani katika kuwasaidia wazee na wasiojiweza huku wakiiomba serikali kuangalia namna ya kupunguza changamoto zinazowakabili wazee.
Awali akisoma risala kwa niaba ya wazee hao mbele ya Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli, Afisa Maendeleo wa Jamii Lidiana Kasheku amemueleza Mama Janeth namna Halmashauri hiyo ilivyojipanga kutatua kero za wazee hao ikiwa ni pamoja na kuanzisha Baraza la Wazee litakalosaidia kubaini changamoto na aina ya msaada wanaouhitaji sambamba na kutoa kipaumbele kwa wazee katika huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na suala la matibabu kwa wazee.
Mama Janeth Magufuli amekabidhi vitu mbalimbali ikiwa ni pamoja na Mchele, Unga wa Mahindi,Mafuta ya Kula, Sabuni za kufulia na Maharage.
Wilaya ya Chato mkoani Geita ina vijini 115 vyenye wazee zaidi ya 18,000 ikiwa ni sawa na asilimia 5 ya wazee wote nchini barani Afrika.
Post a Comment
Post a Comment