Tangu kuingia madarakani kwa Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli ambaye amekuja na kasi ya kutumbua na kurekebisha mfumo wa ufanyaji kazi kwa watumishi wa serikali, baadhi ya wateule wake wameonekana wakishindana katika kuweka watu rumande kwa saa 48, watu wanaowatuhumu kufanya makosa mbalimbali, hasa viongozi wa kisiasa wa vyama vya upinzani.
Matukio haya yamekuwa yakizua malalamiko mengi kutoka vyama vya upinzani na wanaharakati nchini na manung’uniko ya chini kwa chini kutoka kwa wananchi wanaofatilia siasa za nchi hii.
Pengine wengi wanatoa manung’uniko hayo kwa kutumia akili ya kawaida tu ya kibinadamu (common sense) ambayo wanadhani ingetumika kabla hata ya kutoa amri husika.
Ifuatayo ni tafsiri ya Sheria inayompa mamlaka Mkuu wa Mkoa na Wilaya kutoa amri ya mtu yeyote kukamatwa na kuwekwa rumande kwa muda usiozidi saa 48. Pamoja na mamlaka hayo, pia Sheria hii imeeleza mipaka ya Mkuu wa Mkoa na Wilaya juu ya amri hiyo. Soma zaidi upate kuielewa:
Ibara ya Saba (7)
Mamlaka ya Mkuu wa Mkoa
(1) Kwa malengo ya kutimiza majukumu yake kwa ufanisi kwa mujibu wa Sheria hii, Mkuu wa Mkoa anayo Mamlaka ya kuamrisha mtu yeyote akamatwe ambaye (Mkuu wa Mkoa) anaona kuwa amefanya kosa lolote ambalo litamfanya mtu akamatwe na kushtakiwa.
(2) Pamoja na yaliyoelezwa kwenye kifungu cha (1), endapo Mkuu wa Mkoa atakuwa na sababu za kuamini kuwa mtu yeyote ana uwezekano wa kusababisha uvunjifu wa amani au kuondoa utulivu kwenye jamii, au kufanya jambo lolote ambalo kwa namna yoyote linaweza kusababisha uvunjifu wa amani au kusababisha vurugu, na vurugu au uvunjifu huo wa amani hauwezi kuzuilika kwa njia nyingine yoyote zaidi ya kumuweka kizuizini anayesababisha hali hiyo, anaweza kumuamuru ofisa wa Polisi yeyote kwa maneno au kwa maandishi – amkamate mtu huyo.
(3) Mtu aliyewekwa kizuizini kutokana na mamlaka yaliyotolewa kwenye ibara hii, mapema iwezekanavyo, na kwa namna yoyote ile katika kipindi kisichozidi saa arobaini na nane tangu kukamatwa kwake, anatakiwa kufikishwa mahakamani ili asomewe mashtaka yanayomkabili kwa mujibu wa Sheria kwa makosa anayotuhumiwa.
(4) Kama mtu aliyekamatwa kwa amri ya Mkuu wa Mkoa kwa mujibu wa mamlaka aliyopewa na Ibara hii hajafikishwa mahakamani na Mkuu wa Mkoa ndani ya saa arobaini na nane tangu kukamatwa kwake, anatakiwa, muda huo wa saa arobaini na nane utapokwisha, aachiwe huru na asikamatwe tena kwa amri ya Mkuu wa Mkoa huyo akimtuhumu tena mtu huyo kwa kosa kama hilo.
(5) Iwapo Mkuu wa Mkoa ataamrisha kukamatwa kwa mtu yeyote kwa mujibu wa mamlaka aliyopewa na ibara hii, (Mkuu wa Mkoa huyo) anatakiwa wakati anatoa amri hiyo au mapema iwezekanavyo baada ya kutoa amri hiyo, atoe taarifa ya maandishi akieleza sababu zake za kumkamata au kutoa amri ya kukamatwa kwa mtu husika; na anatakiwa kuwasilisha nakala ya sababu hizo, (au hiyo) kwa Hakimu katika muda ambao mtu huyo anafikishwa mahakamani, au, iwapo mtu huyo atakuwa ameachwa huru kabla hajafikishwa mahakamani, (nakala hii iwasilishwe) mapema iwezekanavyo baada ya kuachiwa kwa mtu huyo; na kwa kuondoa mashaka, Hakimu atakuwa na mamlaka ya kuamuru kuachiwa na kuwekwa huru kwa mtu yeyote aliyefikishwa mahakamani bila kutolewa sababu rasmi za kukamatwa kwake, na kuamuru amri hiyo (ya Mkuu wa Mkoa) ifutwe kimaandishi na Mkuu wa Mkoa mwenyewe au na mtu mwingine kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huyo.
(6) Pamoja na yaliyoelezwa kwenye kifungu cha (5), kuwasilishwa kwa nakala ya sababu ya kutolewa kwa amri hiyo kwa mujibu wa mamlaka yaliyotolewa na ibara hii hakumuamrishi Hakimu kusimamia/kutekeleza amri hiyo ya Mkuu wa Mkoa bali Hakimu atamtaka (Mkuu wa Mkoa) atoe nakala hiyo chini ya kiapo.
(7) Hakimu ambaye mtuhumiwa huyo atapelekwa mbeye yake kutokana na kutumika kwa mamlaka hii, anaweza, atakapoona inafaa, kumuweka rumande mtu huyo mpaka kukamilika kwa uchunguzi kwa mujibu wa ibara ya 79 ya Sheria ya Makosa ya jinai bila chuki dhidi yake au anaweza kwa mamlaka ya Mahakama, kumpa dhamana mtuhumiwa huyo kama akiona inafaa.
(8) Kila Mkuu wa Mkoa na kila polisi au mtu yeyote aliyehusika kutekeleza amri hiyo ya Mkuu wa Mkoa kama alivyopewa kwenye ibara hii anatakiwa pia kutekeleza amri yoyote itakayotolewa na Hakimu kwa mujibu wa ibara hii endapo ataamua kumuachia huru mtu huyo aliyekamatwa kwa kutumia mamlaka yaliyotolewa na ibara hii, na kushindwa au kudharau kutekeleza amri hiyo atakuwa amefanya kosa la kuidharau Mahakama na ataadhibiwa kisheria kwa mujibu wa ibara ya 114 ya Sheria ya Adhabu.
(9) Endapo Mkuu wa Mkoa atatumia nguvu aliyopewa na ibara hii vibaya, kwa kutumia vibaya mamlaka ya ofisi yake, hivyo basi yeye, pamoja na mtu yeyote yule aliyehusika kumpa Mkuu wa Mkoa taarifa zilizosababisha matumizi mabaya ya madaraka, atakuwa na hatia ya kufanya kosa hili na anaweza kushtakiwa kwa mujibu wa ibara ya 96 ya Sheria ya Adhabu.
Ibara yaKumi na tano (15)
Mamlaka ya Mkuu wa Wilaya
(1) Kwa malengo ya kutimiza majukumu yake kwa ufanisi kwa mujibu wa Sheria hii, Mkuu wa Wilaya anayo mamlaka ya kuamrisha mtu yeyote akamatwe ambaye anaona kuwa amefanya kosa lolote ambalo litamfanya mtu akamatwe na kushtakiwa.
(2) Pamoja na yaliyoelezwa kwenye kifungu cha (1), endapo Mkuu wa Wilaya atakuwa na sababu za kuamini kuwa mtu yeyote ana uwezekano wa kusababisha uvunjifu wa amani au kuondoa utulivu kwenye jamii, au kufanya jambo lolote ambalo kwa namna yoyote linaweza kusababisha uvunjifu wa amani au kusababisha vurugu, na vurugu au uvunjifu huo wa amani hauwezi kuzuilika kwa njia nyingine yoyote zaidi ya kumuweka kizuizini anayesababisha hali hiyo, anaweza kumuamuru ofisa wa Polisi yeyote kwa maneno au kwa maandishi – amkamate mtu huyo.
(3) Mtu aliyewekwa kizuizini kutokana na mamlaka yaliyotolewa kwenye ibara hii, mapema iwezekanavyo, na kwa namna yoyote ile katika kipindi kisichozidi saa arobaini na nane tangu kukamatwa kwake, anatakiwa kufikishwa mahakamani ili asomewe mashtaka kwa mujibu wa makosa anayotuhumiwa kuyafanya.
(4) Kama mtu aliyekamatwa kwa amri ya Mkuu wa Wilaya kwa mujibu wa mamlaka aliyopewa na Ibara hii hajafikishwa mahakamani na Mkuu wa Wilaya ndani ya saa arobaini na nane tangu kukamatwa kwake, anatakiwa, muda huo wa saa arobaini na nane utapokwisha, aachiwe huru na asikamatwe tena kwa amri ya Mkuu wa Wilaya huyo akimtuhumu tena mtu huyo kwa kosa kama hilo.
(5) Iwapo Mkuu wa Wilaya ataamrisha kukamatwa kwa mtu yeyote kwa mujibu wa mamlaka aliyopewa na ibara hii, (Mkuu wa Wilaya huyo) anatakiwa wakati anatoa amri hiyo au mapema iwezekanavyo baada ya kutoa amri hiyo, atoe taarifa ya maandishi akieleza sababu zake za kumkamata au kutoa amri ya kukamatwa kwa mtu husika; na anatakiwa kuwasilisha nakala ya sababu hizo, (au hiyo) kwa Hakimu katika muda ambao mtu huyo anafikishwa mahakamani, au, iwapo mtu huyo atakuwa ameachwa huru kabla hajafikishwa mahakamani, (nakala hii iwasilishwe) mapema iwezekanavyo baada ya kuachiwa kwa mtu huyo; na kwa kuondoa mashaka, Hakimu atakuwa na mamlaka ya kuamuru kuachiwa na kuwekwa huru kwa mtu yeyote aliyefikishwa mahakamani bila kutolewa sababu rasmi za kukamatwa kwake, na kuamuru amri hiyo (ya Mkuu wa Wilaya) ifutwe kimaandishi na Mkuu wa Wilaya mwenyewe au na mtu mwingine kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya huyo.
(6) Pamoja na yaliyoelezwa kwenye kifungu cha (5), kuwasilishwa kwa nakala ya sababu ya kutolewa kwa amri hiyo kwa mujibu wa mamlaka yaliyotolewa na ibara hii hakumuamrishi Hakimu kusimamia/kutekeleza amri hiyo ya Mkuu wa Wilaya bali Hakimu atamtaka (Mkuu wa Wilaya) atoe nakala hiyo chini ya kiapo.
(7) Hakimu ambaye mtuhumiwa huyo atapelekwa mbeye yake kutokana na kutumika kwa mamlaka hii, anaweza, atakapoona inafaa, kumuweka rumande mtu huyo mpaka kukamilika kwa uchunguzi kwa mujibu wa ibara ya 79 ya Sheria ya Makosa ya jinai bila chuki dhidi yake au anaweza kwa mamlaka ya Mahakama, kumpa dhamana mtuhumiwa huyo kama akiona inafaa.
(8) Kila Mkuu wa Wilaya na kila polisi au mtu yeyote aliyehusika kutekeleza amri hiyo ya Mkuu wa Wilaya kama alivyopewa kwenye ibara hii anatakiwa pia kutekeleza amri yoyote itakayotolewa na Hakimu kwa mujibu wa ibara hii endapo ataamua kumuachia huru mtu huyo aliyekamatwa kwa kutumia mamlaka yaliyotolewa na ibara hii, na kushindwa au kudharau kutekeleza amri hiyo atakuwa amefanya kosa la kuidharau Mahakama na ataadhibiwa kisheria kwa mujibu wa ibara ya 114 ya Sheria ya Adhabu.
(9) Endapo Mkuu wa Wilaya atatumia nguvu aliyopewa na ibara hii vibaya, kwa kutumia vibaya mamlaka ya ofisi yake, hivyo basi yeye, pamoja na mtu yeyote yule aliyehusika kumpa Mkuu wa Wilaya taarifa zilizosababisha matumizi mabaya ya madaraka, atakuwa na hatia ya kufanya kosa hili na anaweza kushtakiwa kwa mujibu wa ibara ya 96 ya Sheria ya Adhabu.
ASANTE KWA KUTEMBELEA MTANDAO WETU!!
Post a Comment
Post a Comment