Kampuni namba moja kwa uchimbaji wa dhahabu duniani, Barrick Gold Corp imesema kuwa inatarajia kuanza kufanya mazungumzo na serikali ya Tanzania kuhusu zuio la kusafirisha mchanga wa madini (makinikia) kwenda nje ya nchi.
Barrick ambao ndio wanahisa wakubwa wa Kampuni ya Acacia yenye migodi mitatu nchini Tanzania ilizuiwa kusafirisha makinikia kwa amri ya Rais Dkt Magufuli kuanzia mwezi Machi mwaka huu.
Mazungumzo hayo yanatarajiwa kuanza wiki ijayo, japo kampuni hiyo haikutaja siku kamili.
Barrick imesema kuwa itaendelea kufanya uchunguzi kuhusu zuio hilo na kueleza, madhara yoyote yatakayotokea yatategemea kwa kiasi kikubwa muda ambao zuio la makinikia litakuwepo.
Acacia inayomilikiwa na Barrick kwa asilimia 63.9 imekumbwa na mabadiliko mbalimbali yaliyofanywa katika sheria za usimamizi wa rasilimali kufuatia uamuzi wa Rais Magufuli anayeamini kuwa nchi hainufaiki vya kutosha na sekta ya madini.
Mwenyekiti wa Barrick, Prof. John Thornton alikutana na Rais Magufuli mwezi Juni ambapo walikubaliana kukaa na kutafuta ufumbuzi wa masuala yote.
Post a Comment
Post a Comment