Kwa mara ya kwanza, Kiongozi Mkuu wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe ametofautiana hadharani kimtazamo na aliyekuwa mshauri wa chama hicho, Profesa Kitila Mkumbo ambaye aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Maji.
Profesa Mkumbo na Zitto walitofautiana jana kuhusu Bajeti ya Serikali ya Mwaka wa Fedha 2017/2018 iliyosomwa jana bungeni na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango.
Msomi huyo alikuwa wa kwanza kuandika kwenye akaunti yake ya Twitter akiimwagia sifa bajeti hiyo pamoja na namna ilivyowasilishwa na Dk. Mpango, akieleza kuwa ni bajeti safi na kwamba anajivunia kuwa sehemu ya timu iliyoiwasilisha.
Hata hivyo, Zitto aliibuka na mawazo kinzani akieleza kuwa bajeti hiyo haitekelezeki, huku akikumbusha kuwa katika bajeti iliyopita ni asilimia 30 pekee ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya maendeleo zilitolewa na kwamba asilimia 20 ya fedha hizo zilipotea.
Jana, idadi kubwa ya wabunge walionesha kuipokea kwa furaha kuu bajeti iliyosomwa na Dk. Mpango ambayo pamoja na mambo mengine ilitaja kuondoa ada ya mwaka ya leseni ya magari, kupunguza kodi ya bidhaa za mazao huku ikipandisha kodi ya mafuta na bia.
Post a Comment
Post a Comment