KATIKA mwaka wa fedha 2017/18, serikali imesema itawatambua rasmi wafanyabiashara wadogo wadogo wasio rasmi kwa kuwapatia vitambulisho maalumu vya kazi wanazozifanya.
Akiwasilisha Bungeni mapendekezo ya serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2017/18, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, alisema jana mbali na kupatiwa vitambulisho maalum pia watatengewa maeneo.
Alisema wafanyabiashara hao ni pamoja na mama lishe, wauzaji mitumba wadogo, wauza mazao ya kilimo wadogo kama mboga mboga, ndizi, matunda na kadhalika.
Biashara zafungwa
Akizungumzia kuhusu kufungwa kwa biashara, Dk. Mpango alisema jumla ya biashara 7,277 zilifungwa katika mikoa mbalimbali nchini kwa mwaka wa fedha unaomalizika Juni 30.
Alisema suala hilo lilizungumzwa sana na wananchi na wabunge kutokana na kasi ya kufungwa kwa biashara hususan eneo la Kariakoo katika Jiji la Dar es salaam na katika miji mingine.
“Kwa mujibu wa taarifa zilizofikishwa TRA, katika kipindi cha kuanzia julai 2016 hadi machi 2017, jumla ya biashara 7,277 zilifungwa katika mikoa mbalimbali nchini,” alisema.
Alibainisha kuwa mwenendo huo kwa ujumla siyo mzuri kwasababu wananchi wanapoteza ajira na kipato, serikali inakosa mapato ya kodi na uchumi unadorora.
Alisema ni muhimu pale wimbi la kufungwa kwa biashara linapotokea jitihada zifanyike kuelewa aina gani za biashara zinafungwa, kwanini zinafungwa na hatua gani zichukuliwe kudhibiti hali hiyo.
Aidha alisema zipo sababu nyingi zinazoweza kuwa zimepelekea hali hiyo, ikiwa ni pamoja na ushindani mkali wa kibiashara, usimamizi dhaifu wa biashara, kuongezeka kwa gharama za kufanya biashara kama vile usafirishaji, kodi na tozo mbalimbali.
Post a Comment
Post a Comment