Swali: Tumeona kuwa sasa hivi Rais anachukua watu kutoka upinzani na kuwapa nafasi katika serikali yake, unalichukuliaje hili?
Lissu: Hao sio wapinzani na hawajawahi kuwa wapinzani, walianzishwa kwa ajili ya kuua upinzani – imeshindikana na sasa wanazawadiwa. ACT na Anna Mghwira walikuwa wakabiliane na Lowassa, sio wakabiliane na CCM, walipata kura elfu tisini na ngapi sijui hawakufika hata kura laki moja. Sasa, huu ukuu wa mkoa ni zawadi tu. Ukatibu mkuu wa Kitila Mkumbo ni kuwazawadia watu wao. Serikali ya Chama Cha Mapinduzi haijawahi kuwa na shida na ACT, haijawahi kuwa na shida na Anna Mghwira, haijawahi kuwa na shida na Kitila Mkumbo na haijawahi kuwa na shida na ‘hao wote wanaojiita wapinzani.’ Shida yao kubwa ni CHADEMA, shida yao kubwa ni CUF. Hao ndio wapinzani, wengine wote hawa ni wana CCM. Wengine wamevaa gwanda hili, wengine wamevaa gwanda lile. Wote ni wana CCM kwa sababu wanafanya kazi za CCM.
Swali: Labda itokee Mh. Rais amekuteua kwenye nafasi yoyote ile ambayo ana mamlaka nayo, itakuwaje?
Lissu: Kwanza haitatokea, nikutoe wasiwasi. Pili, hata ikitokea Rais akafanya hivyo, nitamwambia mheshimiwa mimi napinga mfumo uliokuweka madarakani. Tunataka Katiba mpya, tunataka tutengeneze nchi upya. Kwahiyo kwanza hawezi na pili akinijaribu nitamwambia wazi kwamba kama unataka niitumikie nchi hii tubadilishe Katiba na tuiweke nchi sawa kwenye misingi sawa. Lakini mimi siwezi kutumikia utawala wa kidikteta kwa nafasi yoyote ile. Mimi ni mpinzani, na ndio maana nipo Mahakamani kila siku. Wanaopewa hizo nafasi sio wapinzani, ni watu wanaotumiwa kuua upinzani na hawataweza.
Post a Comment
Post a Comment