Spika wa Bunge Mhe. Job Ndugai ameonyesha kuumizwa na kitendo cha baadhi ya wabunge wa upinzani kutojumuika pamoja na wabunge wenzao katika masuala ya kijamii ikiwepo kususia futari iliyokuwa imeandaliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Kufuatia jambo hilo Ndugai amewaomba viongozi na wabunge kwa pamoja kuachana na mambo ya kujitenda kwani yanaweza kuleta athari kubwa ambazo hakuna anayehitaji, na kudai kama kuna mambo ambayo yanakwaza basi viongozi hao wanapaswa kukaa pamoja na kumaliza mambo hayo.
"Tumekuwa tukiandaa baadhi ya hizi shughuli siku ile ya bajeti tulipata nafasi ya kupata futari iliyokuwa imeandaliwa na Waziri Mkuu na wageni wote waliokuwepo, mabalozi tulihudhuria pale na ilikuwa imeandaliwa kwa wema kwa kweli. Leo (jana) pia na mimi nimepata nafasi ya kuandaa kama nilivyowataarifu lakini nikajifunza kitu kimoja ambacho sikupenda kukisema lakini ngoja nikiseme hapa kidogo, kuna baadhi yetu wengine wamekatazana rasmi kutohudhuria shughuli kama hizi, sasa mimi sitaki kuingilia uhuru wao, wana haki kufanya hivyo kama wanaona ni sawa lakini mimi mwenzao ningependa kuwashauri tu hasa viongozi wanaofanya mambo hayo kutazama tena njia zao, yako mambo mengine ni ya kijamii tu, ukifika mahali kiongozi unaanza kuwazuia watu hata mambo ya kijamii ujue unaenda mbali kidogo" alisema Ndugai
Spika wa Bunge aliendelea kutoa malalamiko yake dhidi ya vitendo vya baadhi ya wabunge wa upinzani kususia shughuli hizo za kijamii ambazo zinawaweka pamoja na kusema
"Hili bunge linavyoendeshwa labda wabunge wa kambi mbalimbali mnaweza msielewe bunge hili linaendeshwa katika mawasiliano mbalimbali ya sisi kwa sisi endapo kuna jambo linakwaza mpaka linasababisha hata watu wasipate futari kwa pamoja basi ni vizuri viongozi wa pande zote tukakaa tuzungumze na kuondoa vikwazo hivyo kama vipo maana mimi sijui kama vipo lakini kama havipo ni vizuri tuwe tunajumuika kwa pamoja, maana sera hizo zikienea na hakika kabisa na pande zingine nazo zitaanza na hakika matokeo yake italeta mipasuko ambayo hakuna anayehitaji hapa" alisisitiza Job Ndugai
Ndugai alisema kuwa yeye anatambua kuwa wanamjibu na kufanya wanayoyafanya lakini Mungu anajua kuwa wanachokifanya si busara kwa kufanya hivyo na kusema kuwa katika mwezi huu mtukufu wanapaswa kusameheana, kuombeana, kutoa mikono upande wa pili na kufanya ibada kwani si mwezi wa chuki na kubaguana.
Post a Comment
Post a Comment