WAKATI mshambulizi Mganda, Emmanuel Okwi anahitaji zaidi ya milioni 100 za kitanzania ili kurejea klabuni Simba kwa uhamisho wake wa tatu, wachezaji walioisaidia timu hiyo kupata ubingwa wa kombe la FA msimu uliopita wanaendelea kuzungushwa kuhusu malipo yao ya mshahara wa mwezi wa tano, pia hakuna bonasi yoyote ile ambayo uongozi wa klabu hiyo umetoa kwa wachezaji.
Viongozi wa klabu badala ya kuboresha kikosi chao wamekuwa ‘bize’ kusaka wachezaji wanaowapenda na si wale waliopendekezwa na kocha Mcameroon, Joseph Omog.
Okwi si chaguo la Omog, na kocha huyo hakupendekeza usajili wa aliyekuwa nahodha wa Azam FC, John Bocco pia alimuhitaji Ally Shomari kutoka Mtibwa Sugar FC kama mbadala na msaidizi wa Mcongoman, Javier Besala Bokungu katika beki ya kulia lakini uongozi umetoa Tsh. milioni 60 na kumsaini Shomari Kapombe kutoka Azam FC.
Huu ni usajili wa kishabiki zaidi ambao umeendelea kufanywa na kina ‘Mr. Kazinyingi’ wakiongozwa na mwenyekiti wa kamati ya usajili, Zacharia Hans Poppe. Kutoa zaidi ya milioni 200 kwa Okwi, Kapombe na Bocco si sawa kwa timu kama Simba hasa ukizingatia wachezaji hao wote watatu hawajapendekezwa na kocha.
Pia kuendelea kung’ang’ani saini yenye thamani ya zaidi ya milioni 100 ya Mnyarwanda, Haruna Niyonzima kutoka Yanga wakati si pendekezo la mwalimu ni sawa na ‘ujinga’ ambao ukuapo huzalisha ‘upumbavu.’
Ni kweli, Simba inahitaji wafungaji wawili wa nyongeza katika kikosi chao hasa baada ya kumpoteza Ibrahim Ajib, pia kikosi hicho kimepatia sana kuwasaini mlinda mlango, Aishi Manula kutoka Azam FC, Ally Shomari na beki namba 3, Jamaly Mwambeleko kutoka Mbao FC.
Pia usajili wa beki ya kati unahitajika licha ya kumsaini, Yusuph Mlipili kutoka Toto Africans ila katika eneo la kiungo, Omog hana upungufu mkubwa ambao unapelekea klabu kuhitaji saini mpya yenye thamani ya zaidi ya milioni 100.
Nahodha, Jonas Mkude, Mghana, James Kotei, Muzamiru Yassin, Mohamed Ibrahim hawa ni viungo wanne wa kati wenye uwezo wa juu.
Ili kujenga timu yenye ubora ni heri pesa aliyotumika kumsaini Kapombe ingefanya kazi hiyo kumleta kikosi Mrundi, Yusuph Ndikumana ambaye si tu ni beki mzuri wa kati bali ni chaguo la kocha Omog ambaye anamuhitaji beki huyo wa kati wa Mbao FC ili kushirikiana na Mganda, Juuko Murishid.
Kuna wakati nilimsikia Hans Poppe akisema hawawezi kumsaini tena Ndikumana kutokana na mchezaji huyo kuhitaji dau la juu ( Tsh. milioni 60) lakini naamini aliamua kumpuuza mchezaji huyo kwa sababu ni chaguo la Omog si yeye wala kamati yake ndio maana licha ya kutohitajika na kocha, Bocco, Kapombe na pengine Okwi ‘wataikwangua’ klabu hiyo zaidi ya milioni 200.
Simba inapaswa kuwasaini, Ndikumana au Salim Mbonde kutoka Mtibwa Sugar ili kuimarisha beki yao ya kati. Wanapaswa kuendelea kuwashikilia Abdi Banda na Juuko huku pia wakisaini wafungaji ambao wamependekezwa na Omog.
Kuendelea ‘kufuja’ pesa ‘wanazokopeshwa‘ na mfadhili wao ni sawa na kuiangusha klabu kiuchumi na kuharibu ufanisi wa timu iliyoanza kujengwa vizuri ndani ya uwanja.
Najiuliza, Okwi, Bocco, Kapombe wa nini Simba SC wakati hawawezi kuziba nyufa zilizowaangusha msimu uliopita.?
Narudia kutolea mfano usajili wa timu hiyo mwishoni mwa mwaka 2002, ambapo aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Mkenya, James Siang’a (Mwenyezi Mungu amerehemu) licha ya kusajiliwa kwa wachezaji kwa nyota kama Ulimboka Mwakingwe, Lubigisa Madata, Victor Costa, Christopher Alex (Mwenyezi Mungu amerehemu,) kocha huyo alimwambia wazi aliyekuwa katibu mkuu wa klabu wakati huo, Kassim Dewji,
“Bila kuwasaini Primus Kasonso na Juma Kaseja naacha kazi…”Omog anasubiri nini wakati mapendekezo yake yametimizwa kwa Manula, Ally na Mwambeleko tu? Ndiyo maana nilisema awali kocha huyu hafai Simba SC.
Wakati ule niliposema barua ya Simba kwenda FIFA haikuwa na mashiko zaidi ya kutafuta ‘chaka’ la uongozi kufichia madhaifu yao, kuna baadhi ya wasomaji walipinga sana. Nauliza, vipi kombe la Simba limeshafika kutoka FIFA? Sasa wanawapotezea mbali kwa sajili za Mr. Kazinyingi.
Hakika naona Simba SC wakijiandalia anguko lao jingine, sababu kina Okwi, Niyonzima, Bocco, Kapombe si sajili za Omog…
Post a Comment
Post a Comment