WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali imefanikiwa kuokoa Sh bilioni 53.9 kutokana na uchunguzi na operesheni mbalimbali zilizofanywa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) katika mwaka 2016/2017.
Amesema kiasi hicho cha fedha ni kikubwa mno, ikilinganishwa ni Sh bilioni 7 tu zilizookolewa katika mwaka 2015/2016. Alisema hayo jana wakati akifungua semina ya Mtandao wa Wabunge wa Afrika walio katika Mapambano ya Rushwa (APNAC) Tawi la Tanzania kwenye ukumbi wa African Dream mjini Dodoma.
Akizungumzia hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali katika mapambano dhidi ya rushwa, alisema Serikali imeanza kupata mrejesho mzuri kwamba watumishi wa umma wanawajibika ipasavyo na vitendo vya rushwa vinaendelea kupungua.
“Baadhi ya hatua tulizochukua ni pamoja na kuimarisha taasisi yetu ya TAKUKURU; kuimarisha matumizi ya mashine za kielektroniki ili kupunguza mianya ya kupoteza mapato; kuanzisha mahakama ya mafisadi; kusimamia nidhamu katika utumishi wa umma na kuchukua hatua za haraka za kinidhamu na za kisheria dhidi ya watuhumiwa wote wa rushwa na ufisadi,” alisema.
Aliwaomba wabunge waendelee kuiunga mkono Serikali, kwani haina mzaha kwenye mapambano hayo. “Serikali haina mzaha kwenye mapambano dhidi ya rushwa na tutaendelea na mapambano hayo.
Hivyo, ninaomba waheshimiwa wabunge muendelee kutuunga mkono katika mapambano haya, twende kwa wananchi tukatoe wito kwao watuunge mkono kwenye vita hii,” alisisitiza.
“Tayari tumefanya tathmini na kubaini mianya ya rushwa katika sekta za ardhi, uchukuzi, biashara na maji na hivyo kuziba mianya hiyo. Tutaendelea kuiwezesha TAKUKURU ili iendelee na kazi nzuri waliyoianza ya kubaini mianya na kutoa ushauri wa kuziba mianya hiyo ya rushwa.
Lengo letu ni kuwekeza zaidi kwenye kuzuia, kwa kuwa kinga ni bora kuliko tiba”. Mapema, akizungumza katika semina hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki alisema Takukuru kwa kushirikiana na taasisi zilizo chini yake, wako njiani kuanzisha mtaala wa somo la rushwa ili ifundishwe tangu shuleni.
“Napenda kuwahakikishia waheshimiwa wabunge kwamba Serikali ya awamu ya tano haitakubali kuona rushwa ikiota mizizi. Tunaamini wanafunzi wakijengewa uwezo tangu utotoni, watachukia rushwa na hatimaye tutakuwa na Taifa lenye watu waadilifu,” amesema.
Alisema kutokana na kazi ya kupunguza watumishi hewa, hadi kufikia Aprili mwaka huu, Serikali imekwishapokea Sh bilioni 1.2 kwenye akaunti maalumu ya Takukuru iliyoko Hazina ambazo zinatokana na makusanyo kutoka kwa waliokuwa watumishi hewa.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkazi wa UNDP, Godfrey Mulisa alisema wataendelea kushirikiana na Bunge katika miradi mbalimbali ikiwemo shughuli zinazofanywa na APNAC.
Awali, Mwenyekti wa APNAC tawi la Tanzania, George Mkuchika alisema hadi sasa wabunge wapatao 148 wamekwishajiunga na mtandao huo. Kwamba anaamini hadi Bunge hili litakapomaliza muda wake, zaidi ya robo tatu ya wabunge watakuwa wamejiunga
Post a Comment
Post a Comment