NI jambo lisilohitaji mjadala, kukubaliana kwamba Rose Muhando, ni mmoja wa watu ambao Muziki wa Injili Tanzania, una damu yake, hasa unapozungumzia kile kitendo cha kuutoa ndani ya nyumba za ibada na kuuleta nje, tena kwenye majukwaa.
Ndiyo, Gospo ni muziki wa ndani ya nyumba za ibada, ukipigwa na wanakwaya kwa miaka mingi hapa kwetu na ilipolazimika kutoka nje, basi ni kwenye matamasha ya shughuli za kidini na hakukuwahi kuwa na mtu mmoja aliyeweza kusimama peke yake kuimba.
Lakini Rose Muhando ni miongoni mwa waimbaji wa kwaya walioamini wanaweza kufanya vitu viwili kwa wakati mmoja, kuimba kwa kumsifu Mungu, lakini wakati huo huo wakajiingizia kipato.
Alifanya hivyo na akakubalika sana, kwani mashabiki wa nyimbo zake hawakuwa watu wa kanisani tu, hata watu wa imani nyingine walivutiwa na nyimbo zake.
Ndiye aliyekuwa kioo cha waimbaji wengine kujitokeza na kuonyesha uwezo wao, kiasi kwamba wengi wakaanza kumtumia kama chanzo cha mapato, akiitwa huku na kule kutumbuiza katika matamasha na zinduzi mbalimbali za albamu na nyimbo za wanakwaya wenzake.
Ukubwa wa jina na kazi yake ukawavutia hadi watu wa Sony Music ambao waliweza kuingia naye mkataba wa kumsimamia katika shughuli zake za muziki.
Kuwavutia watu kama Sony siyo jambo dogo, maana hawa jamaa wanafanya kazi kimataifa na wako na wasanii wengi dunia nzima. Achana na tuhuma za utumiaji wa madawa ya kulevya, acha ile ya maneno kuwa anazaa nje ya ndoa, maana hivi vitu ni kwa faida yake, afanye, asifanye shauri yake na maisha yake.
Lakini kuna hili jambo ambalo mwanzo lilianza kama tetesi, baadaye ikaja kujulikana kuwa ni kweli. Binafsi nimeshawahi kuzungumza naye juu ya hili jambo, akakataa kabisa, akitoa madai kuwa kuna watu wamejipanga kumchafua na anawajua. Ni hili la utapeli katika shoo zake.
Tuhuma zinasema Rose anachukua hela kwa ajili ya kushiriki matamasha ya nyimbo, lakini hatokei. Nimekutana na watu wengi wanaomlalamikia kuhusu tabia yake hii, ambayo tofauti na yale mawili ya mwanzo, hili ni jinai, linaweza kumfunga jela.
Post a Comment
Post a Comment