Mkurugenzi wa Kampuni ya Victoria Media Services Ltd ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa gazeti la MAWIO lililofungiwa kwa miezi 24 (miaka 2) amesema kuwa amepokea simu za vitisho kutoka kwa watu asiowafahamu.
Simon Martha Mkina aliyasema hayo jana alipokuwa akifanya mahojiano na Shirika la Habari la Ufaransa, AFP kuwa amepokea takribani simu tatu za vitisho ikiwa ni siku chache tangu serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ilipolifungia gazeti la MAWIO.
Simon Mkina (katikati) alipokuwa akitoka Kituo cha Polisi Dar es Salaam. (Picha ya maktaba)
Mkina alisema kuwa miongoni mwa simu hizo tatu, moja ilikuwa sauti ya mwanaume ambapo alimtisha na kukata simu. Alisema kuwa haikuonyesha namba yake hivyo hakuweza kumpigia tena ili kuweza kujua sababu za kumtisha na yeye ni nani.
Mkina alisema kuwa alitoa taarifa kituo cha Polisi ambapo walimwambia itakuwa vigumu kufanya jambo lolote kwa sababu simu hizo zilipigwa na watu wasiofahamika na namba zao hazifahamiki.
Uamuzi wa kulifungia gazeti hilo ulitangazwa Wizara ya Habari ambapo sababu iliyotajwa ni gazeti hilo kukiuka maagizo ya serikali ya kutowahusisha marais wastaafu Mzee Mkapa na Dkt Kikwete katika ripoti za uchunguzi wa mchanga wa madini.
Hii ni mara ya pili kwa gazeti hilo kufungiwa kwani, Januari 2016 aliyekuwa Waziri wa Habari, Nape Nnauye alitangaza kulifungia kwa muda usiojulikana baada ya kuchapisha habari iliyodaiwa ni ya uchochezi. Habari hiyo ilikuwa na kichwa cha habari kinachosomeka “Machafuko yaja Zanzibar.” Uamuzi huo ulipingwa na Mahakama Kuu ya Tanzania, Machi mwaka huu na gazeti hilo kurejea mtaani kabla ya kufungiwa tena.
The Citizen
Post a Comment
Post a Comment