Pyongyang, Korea Kaskazini. Korea Kaskazini imesema makombora iliyoyafanyia majaribio jana Alhamisi ni mahsusi kwa ajili ya kushambulia ‘kundi la meli za kivita’ ambazo zimekuwa zikiitishia nchi hiyo.
Shirika la Habari la Serikali la KCNA limesema majaribio hayo ya jana ya makombora ya ardhini kwenda baharini ni ya hivi karibuni katika msururu wa vitendo vya ukiukaji wa vikwazo vya Umoja wa Mataifa na yalishuhudiwa na kiongozi wa nchi hiyo Kim Jong-Un.
Majaribio hayo yamefanyika siku moja baada ya Umoja wa Mataifa kuongeza makali ya vikwazo dhidi ya taifa hilo.
"Makombora hayo yaliyorushwa yaliweza kutambua kwa ufasaha vifaa vilivyolengwa vilivyokuwa vinaelea kwenye bahari ya mashariki mwa Korea," KCNA wamesema, wakizungumzia Bahari ya Japan, ambako kuna meli mbili kubwa za Marekani za kubeba ndege za kivita.
Korea Kaskazini inawezekana inazilenga meli za USS Carl Vinson na USS Ronald Reagan zilizoongoza mazoezi ya siku tatu ambayo yalimalizika Juni 3 yakihusisha meli zaidi ya 10 za kivita za Marekani pamoja na mbili za Japan. Mazoezi hayo yalionekana kulenga kuitisha Korea Kaskazini.
Marekani imezidisha shughuli zake za kuonyesha ubabe wa kijeshi eneo hilo, ambapo ina nyambizi inayotumia nguvu za nyuklia, USS Cheyenne yenye uzani wa tani 6,900.
Post a Comment
Post a Comment