Kwa yeyote aliyewahi kukutana nao, mapacha wawili ambao ni walemavu walioungana matumbo, Maria na Konsolata hatabisha kwamba pamoja na hali yao, watoto hao ni wacheshi, wakarimu na wanaoweza kukufanya utabasamu hata kama moyoni mwako, ulikuwa na huzuni.
Wiki hii walifanyiwa mahojiano na Gazeti la Mwananchi na kufunguka mengi kuhusu maisha yao pamoja na ishu yao ya kufikiria kuolewa.
Si rahisi kufikiria maisha ya ndoa ya Maria na Consolata kwa jinsi walivyo, lakini pacha hawa walioungana wako wazi kuhusu matamanio yao ya maisha ya ndoa.
Katika mazungumzo yao na gazeti hili, Maria na Consolata waliweka bayana mipango yao ya ndoa mara watakapomaliza elimu ya chuo kikuu.
Ingawa ni kitu cha kushangaza, Maria na Consolata hawatakuwa mapacha wa kwanza katika maisha ya ndoa. Chang na Eng Bunker ni pacha wanaume waliozaliwa mwaka 1811 nchini Thailand ambako zamani kuliitwa Siame.
Tofauti na mapenzi ya akina Maria na Consolata, pacha hao kila mmoja alioa mke wake na kufanikiwa kupata watoto.
Kama ilivyokuwa kwa pacha hao, Maria na Consolata wanatamani kuwa wanandoa na ndoto zao ni kuolewa na mwanaume mcha Mungu na atakayewajali.
“Ndoa ni sakramenti takatifu, tukishamaliza masomo yetu ya chuo kikuu tunatamani kuja kuwa wanandoa,” anasema Maria.
Kwa namna walivyo, si rahisi kwao kuolewa na wanaume tofauti isipokuwa mume mmoja na wanalijua hilo.
Haya ndio yalikuwa mahojiano baina yangu na wao kufuatia ndoto hiyo.
Mwandishi: Baada ya masomo, nini ndoto zenu?
Maria: Ndoto zetu ni kuwa wanandoa. Zamani tulikuwa tunapenda tofauti, lakini kwa sasa tumempenda mtu mmoja.
Tumegundua tuna hisia moja.
Mwandishi: Tayari kuna mtu mmempenda nini?
Maria na Consolata kwa pamoja: Ndio tumempenda mtu mmoja.
Mwandishi: Nani alimwambia mwenzake kwanza kuhusu hisia za kupenda?
Consolata: Sisi ndio tuliomwambia kwamba tunampenda, naye alitusikiliza.
Mwandishi: Aliwajibu nini?
Maria: Yupo kwenye tafakari, hawezi kusema akurupuke na kuingia bila tafakari. Lazima tumpe muda wa kutafakari.
Mwandishi: Ni mwanaume wa aina gani mnayempenda?
Consolata; Tunapenda kuolewa na mwanaume wa kawaida, mwenye tabia njema na mcha Mungu asiwe tajiri. Ikiwa tutamaliza masomo yetu, huyu tuliyempenda anafaa kuwa mume wetu. Kihalisia tunatamani mwanaume mcha Mungu, mwenye upendo na ambaye atathamini utu wetu.
Mwandishi: Kwa nini hampendi kuolewa na tajiri?
Consolata: Ni kwa sababu matajiri wengi huwa wanathamini pesa zao sio utu. Samahani hapa sio matajiri wote, ila wengi wao kwa hiyo sisi tunataka mtu anayeweza kuthamini utu.
Mwananchi: Ndoa ni mume na mke mmoja kwa Wakristo. Mmewahi kutafakari hilo?
Consolata; Ndio, Biblia inasema kwamba Mungu aliweka agano kati ya mume na mke mmoja. Sasa kwa kuwa sisi tumeungana wawili na tuna hisia moja, hatuwezi kuolewa na wanaume tofauti. Tutaolewa na mume mmoja.
Tunatamani sana kumtumikia Mungu kupitia sakramenti ya ndoa. Mungu akitujalia tumalize masomo yetu basi tunataka kuolewa ili tumtumikie Mungu katika huo wito vizuri.
Pacha hao waliweka bayana jina la kijana waliyempenda, ingawa kwa sababu za kimaadili tunalihifadhi. Hata hivyo, baba mdogo wa kijana huyo alikuwa tayari kuzungumza na gazeti hili.
Baba huyo mdogo alisema ana taarifa za kijana wao kupendwa na pacha hao.
“Unajua nilishangaa kuona watu wananiita baba mkwe wa akina Maria na Consolata. Baadaye ndio nikajua kuwa kuna mahusiano baina yao (kijana na mapacha hao), japo wote wanaendelea na masomo. Kupenda ni moyo na kama ikitokea wakafikia ndoto hizo huko baadaye, basi itakuwa hivyo,” anasema.
Mwalimu mkuu wa Shule ya Maria Consolata, Jefred Kipingi anasema hisia za kuolewa kwa mabinti hao ni jambo la kawaida na kwamba, wanapenda kuishi maisha ya kawaida kama walivyo watu wengine.
“Uzuri wake ndoto yao ni kuwa walimu na wanasema wataolewa wakishamaliza masomo yao. Jambo hilo ni jema na hapo Mungu ndipo atadhihirisha utukufu wake zaidi,” anasisitiza.
Ingetegemewa kwamba katika dunia ya utandawazi, taarifa za kuzaliwa kwa pacha walioungana zingetapakaa kila mahali zikipamba magazeti, redio, luninga na hata mitandao ya kijamii.
Lakini haikuwa hivyo kwa Maria na Consolata. Hakuna chombo chochote kilichopata taarifa ya kuzaliwa kwa pacha hao wa kipekee.
Ulemavu wao ulisababisha wafichwe hadi walipofikisha umri wa kuandikishwa elimu ya msingi katika Shule ya Ikonda na kutafutiwa mlezi wa kuwaangalia, baada ya wazazi wao kufariki dunia wakiwa wadogo.
Habari zao zilianza kufahamika baada ya kuandikishwa darasa la kwanza na kutafutiwa mlezi aliyewalea hadi wakati walipofaulu vizuri mitihani yao ya darasa la saba mwaka 2010.
Mlezi wao, Bestina Mbilinyi alikuwa alifanya hivyo chini ya wamisionari lakini, alikuwa akiishi nao nyumbani kwake Ikonda.
“Niliombwa niishi na watoto hawa kwa sababu kutoka kwangu hadi shuleni sio mbali, nilijengwa choo kinachokidhi maumbile yao na niliishi nao hadi wanamaliza darasa la saba,” alisema wakati akizungumza na Mwananchi wakati walipomaliza darasa la saba
Post a Comment
Post a Comment