SIRI YA MAFUTA YA TAA KUWEKWA KWENYA CHAKULA SHULE ZA BWENI

Mafuta ya taa ni bidhaa inayotokana na mafuta ya petroli ghafi. Matumizi ya mafuta ya taa katika vyakula vya shule za bweni imekuwa jambo la kawaida katika Afrika Mashariki na nchi nyingine kwa miaka mingi, na imani iliyojengeka ni kuwa yanasaidia kupunguza hamu ya kufanya ngono (libido) kwa wanafunzi walio katika kipindi kigumu mno cha kubalehe (kupevuka). Katika milo yao ya shule za bweni, wanafunzi wamekuwa wakiwekewa dozi za mafuta ya taa kama sehemu ya vyakula pasi na utashi wao.

Baadhi ya shule za Sekondari za bweni nchini zinatuhumiwa kutumia kiasi kidogo cha mafuta ya taa katika chakula cha wanafunzi kwa lengo la kuwapunguzia mihemko ya ngono.

Sekondari kadhaa zikiwamo za Serikali na Seminari zimetajwa kutumia mbinu hiyo, ambayo baadhi ya madaktari wa afya wameeleza kisayansi kuwa mbinu hiyo haisaidii kupunguza tatizo hilo.

Imeelezwa kuwa mbinu ya kutumia mafuta ya taa kwenye chakula inatokana na wanafunzi wengi kujihusisha na ngono, hivyo kujiweka katika hatari ya kukumbwa na magonjwa ya zinaa, kama ukimwi na mimba.

Mmoja wa watu aliyewahi kukumbwa na mbinu hiyo alipokuwa akisoma katika shule ya sekondari ya bweni, alieleza kuwa kwa miaka minne ya masomo alikumbana na milo kadhaa iliyonuka mafuta ya taa.

“Nakumbuka mara kadhaa tuliwashambulia wapishi kwa maneno makali, lakini hakuna sababu ya maana waliyowahi kutujibu. Mara zote walitujibu ni bahati mbaya,” alisema.

Ripoti iliyochapishwa katika jarida la Sayansi la Elsevier kutokana na utafiti uliofanywa na wanasayansi wanne wa nchini Kenya kuhusu matumizi ya mafuta ya taa katika vyakula ili kkupunguza mihemko ya ngono, ulichochewa sana na kuenea kwa taarifa kwamba shule nyingi za bweni katika nchi za Afrika Mashariki na nyinginezo zinatumia mbinu hiyo ili kuwapunguzia wanafunzi hamu ya ngono.

Wanasayansi hao walifanya utafiti wao kwa kuwatumia panya ambao waligawanywa katika makundi matatu. Kundi la kwanza likiwa ni la panya ambao walipewa chakula bila kuwekewa mafuta ya taa, kundi la pili waliwekewa mafuta ya taa kidogo na lile la tatu waliwekewa mafuta ya taa kwa wingi kiasi.

Matokeo ya utafiti yalionyesha kuwa kundi la panya waliowekewa mafuta kidogo kwenye chakula liliongeza ashki kwa 66% na lile lililowekewa mafuta mengi liliongeza ashki kwa 75%.

Hii ina maana kuwa mafuta ya taa yaliongeza ashki badala ya kupunguza, na pia yalisababisha ugonjwa wa gastritis. Ugonjwa huu husababisha madhara ya kuvimba, kuwasha au kumomonyoka kwa kuta za ndani ya tumbo (Stomach lining).

Pia, ripoti hiyo ilibainisha kwamba utafiti wa wanasayansi hao kwa baadhi ya shule za Kenya uligundua wanafunzi waliwekewa mafuta hayo kwenye chakula, lakini yalichochea zaidi ongezeko la mimba, pamoja na vurugu.

Daktari wa magonjwa ya binadamu nchini, gunini Kamba alisemba kwamba ingawa hajaona au kufanya utafiti, ni wazi kuwa mafuta ya taa yana madhara kwa binadamu.

“Mafuta ya taa hayafai kuliwa. Hii siyo mbinu salama kwa afya za hao vijana , bali wanaweza kusaidiwa kwa kukutanishwa kwenye michezo, burudani ikiwemo muziki wakiwa jinsi mbili tofauti wakazungumza na kufurahi pamoja” alisema Dk. Kamba.

Aidha alisisitiza kuwa msaada wa karibu wanaoweza kupewa wanafunzi walio katika umri wa kubalehe ili kuwajengea uelewa wa masuala ya kujamiiana na hali ya kujiamini .

Vile vile kuwafanyisha mazoezi na shughuli zingine zitakazowafanya wakose muda wa kuwaza ngono nayo pia ni mbinu mojawapo inayoweza kutumika kuwasaidia vijana hawa.

Related Posts

Post a Comment