Kauli ya Mbunge wa Misungwi (CCM), Charles Kitwanga kuwa kama Serikali haitashughulikia kilio cha maji jimboni kwake atahamasisha wananchi kubomoa mashine ya Ihelele, imejibiwa.
Aliyetoa majibu hayo ni Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Gerson Lwenge aliyeanza kwa kuhoji iwapo alichosema Kitwanga alitumwa na wapigakura wake.
“Sasa nataka nimuulize Kitwanga kama yupo hapa kwamba hayo ni maneno yake au ya wananchi? Kama ni ya wananchi nitawaambia nini kimefanyika Misungwi kwani hata juzi tumesaini mikataba ya maji na mwenyekiti wa halmashauri alikuwepo ya kupeleka maji Misungwi kutoka Ziwa Victoria kwa fedha nyingi zaidi ya Sh38 bilioni,” alisema.
Lwenge akasema haoni sababu za Kitwanga kushupalia kuharibu miundombinu ya maji kwa sababu Serikali ya Awamu ya Tano imemfanyia mambo makubwa jimboni kwake.
Katika mchango wake, Kitwanga alihoji Serikali kutoshughulikia ipasavyo kilio cha maji kwa wananchi wake na kwamba, fedha ilizotenga kwa ajili ya miradi ya maji ni chache.
“Kwa hiyo, nitakachokifanya safari hii sitatoa shilingi kwenye bajeti, bali nitakwenda kuwahamasisha wananchi wa Misungwi wapatao 10,000, twende tukazime mtambo katika kile chanzo cha maji ili wote tukose,” alisema mbunge huyo.
Pia, Kitwanga alishutumu kuwa kuna mpango wa kumuandaa Bashite kuwa mbunge wa Misungwi.
Post a Comment
Post a Comment