MKAZI wa Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba, Khadija Mbarouk (44), anashikiliwa na polisi kwa madai ya kumuua mumewe kwa sababu zilizoelezwa kuwa ni wivu wa kimapenzi.
Mtuhumiwa huyo inadaiwa alimchoma kisu mumewake baada ya kugundua ameoa mke mwingine.
Inadaiwa baada ya kugundua mume wake, Tani Ali Tani (41), ameoa mke mwingine, alimchoma kisu akiwa nyumbani kwa mke mdogo na kufariki dunia.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kaskazini Pemba, Haji Khamis Haji, alisema tukio hilo limetokea juzi majira ya 2:30 usiku, katika eneo la Kizimbani, Wete Pemba.
Alisema, mwnaume huyo alijeruhiwa baada ya kuchomwa kisu na mkewe katika mguu na kutokwa na damu nyingi na kusababisha kifo chake.
"Khadija alikwenda nyumbani kwa mke mwenziwe (mke mdogo) na kutaka kuzungumza nae na katika mazungumzo yao walianza kugombana na ndipo mwanamke huyo alipochukua hatua ya kumchoma kisu mumewe," alisema.
Alisema kuwa, mara baada ya kujeruhiwa alikimbizwa katika Hospitali ya Wete na ilipofika saa 9:00 usiku alifariki dunia, wakati akipatiwa matibabu.
Alisema mtuhumiwa yuko chini ya ulinzi na upelelezi utakapokamilika, atafikishwa mahakamani kujibu shitaka linalomkabili.
Aidha alisema katika tukio jengine la mauaji, polisi katika mkoa huo, inawashikilia watu watatu wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji ya mtoto mchanga akiwamo mama na baba mzazi wa mtoto huyo akiwamo bibi wa mtoto huyo.
Aliwataja wanaotuhumiwa kuwa ni Riziki Juma (19), mama mzazi wa mtoto, Khamis Hamad Ali (25), baba mazazi na Chumu Matari (bibi wa mtoto).
Kamanda Haji alisema, tukio hilo lilitokea saa 2.00 usiku wa kuamkia Ijumaa baada ya kudaiwa kumuua mtoto huyo kumtupa katika msitu wa mjini Wingwi, Wilaya ya Micheweni Pemba. Inadaiwa watuhumiwa walitumia kitu chenye ncha kali kumuua mtoto huyo mara baada ya kuzaliwa.
Alisema polisi ilipata taarifa hizo kutoka kwa raia wema na kuchukua hatua za kuwatia mbaroni.
Aidha, inadaiwa watuhumiwa hao walitenda kosa hilo kwa lengo la kuficha aibu, kwa madai mama wa mtoto huyo alijifungua ndani ya wiki baada ya kuolewa mwezi uliopita, mwaka huu.
Post a Comment
Post a Comment