MBUNGE wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT), ameeleza namna Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alivyokosolewa na Sir Andy Chande baada ya kumnyang’anya kiwanda.
Zitto ambaye pia ni Kiongozi Mkuu wa ACT Wazalendo, alikumbusha hayo jana katika salamu zake za rambirambi kwa Sir Chande aliyefariki dunia juzi jijini Nairobi Kenya, alikokuwa akitibiwa.
Kwa mujibu wa taarifa yake aliyotoa jana, Zitto alisema Chande ambaye amekuwa Kiongozi mwanachama wa Freemason tangu 1954, alikuwa muathirika wa utaifishaji.
Alisema na Chande alikuwa mmiliki wa viwanda vya kusaga unga ambavyo Nyerere alivitaifisha mwaka 1967 na kuunda Shirika la Usagishaji la Taifa (NMC).
“Mzee Chande ni muathirika wa utaifishaji. Yeye alikuwa akimiliki viwanda vya kusaga unga ambavyo Mwalimu Nyerere alivitaifisha na kuunda NMC.
“Siku ya pili baada ya kuitwa na Waziri wa Biashara Prof. Abdurahman Babu na kuambiwa kuwa Dola imechukua kiwanda chake, aliitwa Ikulu na kufanya mazungumzo na Mwalimu,” alifafanua Zitto.
Alisema Nyerere aliomba radhi kwa uamuzi waliochukua na kueleza kuwa ni muhimu kwa nchi kwakuwa biashara hiyo ya kununua mazao ya kusaga unga, ilikuwa na uhitaji kwa wananchi na kwa mujibu wa Azimio la Arusha ilikuwa lazima kitaifishwe.
Zitto alieleza kuwa baada ya Mwalimu Nyerere kutamka maneno hayo, Chande alimjibu kuwa amefanya makosa makubwa kwa kuwa utaifishaji haukuwa jibu sahihi la matatizo ya kiuchumi ya Tanzania na kwamba historia itawahukumu kwakuwa haikujulikana nani alikuwa sahihi.
Baada ya hapo kwa mujibu wa Zitto, Rais Nyerere alimjibu kuwa asijali kuhusu historia na kumhoji kama anataka kazi serikalini au ubalozini atampa.
Zitto aliendelea kueleza kuwa Chande alimjibu kuwa hataki kazi, bali anataka kuendelea kuendesha kampuni hiyo kwa muda wote atakaoruhusiwa na Nyerere, jambo lililomfanya amjibu kuwa aendelee.
Alifafanua kuwa Mzee Chande aliendelea kuwa Mtendaji Mkuu wa NMC iliyotaifishwa na kuendelea kufanya kazi nyingi nyengine za mashirika ya umma.
Mashirika mengine aliyofanya kazi ni pamoja na kuwa Mwenyekiti wa Bodi wa Shirika la Ndege, Shirika la Reli, Shirika la Magazeti ya Serikali, Bodi ya Utalii na mengine kadha wa kadha.
Zitto aliongeza kuwa hadithi hiyo na nyingine nyingi, Chande ameziweka katika kitabu chake 'Journey from Bukene '.
“Mzee Chande ametangulia mbele ya haki, lakini Mzee Chande amebaki nasi kwani ameandika. Ametuachia historia yake na historia yake ni historia ya nchi yetu pia,” alisema Zitto.
Post a Comment
Post a Comment