Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT –Wazalendo), Zitto Kabwe amesema tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani, taasisi za uwajibikaji ikiwamo Bunge zinashindwa kufanya kazi kutokana na kutopewa fedha za kutosha.
“Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) amenyimwa fedha. Hii inaonyesha kuwa Serikali haina dhamira ya kweli ya kuwezesha Bunge kufanya kazi yake kinyume kabisa na hotuba ya Rais John Magufuli wakati akifungua Bunge Novembea 2015,” amesema Zitto ambaye ni kiongozi wa chama hicho.
Zitto alikuwa akizungumzia taarifa kwamba, chombo hicho cha kutunga sheria kimekumbwa na ukata, kiasi kwamba kina fedha za muda mfupi ujao.
Mbuge wa Ukonga (Chadema), Mwita Waitara ameunga mkono kauli ya mbunge wa Mtwara vijijini, Hawa Ghasia akisema shughuli za Bunge zimedorora.
“Ni kweli kama alivyosema Ghasia kuwa Serikali imeshindwa kutoa fedha za miradi ya maendeleo kwa wizara mbalimbali. Hata kwenye Bunge imeathiri utendaji,” amesema Waitara.
“Kwa mfano katika kamati wabunge wanakwenda kwenye ziara, lakini hawalipwi posho. Wabunge wanakwenda kwenye ziara hawalipwi posho, mwisho kazi zinashindikana kufanyika.
‘Kamati za Bunge zilitakiwa kukaa kwa wiki tatu, lakini zimeishia kukaa wiki moja kwa sababu ya ukata. Wabunge wanashinda mchana kutwa bila kula. Tumemuuliza Spika akasema hakuna hela.”
Juzi, Ghasia ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, alisema wakati ikiwasilisha maoni kuhusu bajeti ya ofisi ya Waziri Mkuu kuwa kumeonekana changamoto kubwa ya Bunge kupewa fedha kwa wakati na hivyo kuathiri utekelezaji wa baadhi ya majukumu.
Post a Comment
Post a Comment