ASKOFU wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amewashukia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, huku akimuelezea msanii wa muziki wa kizazi kipya, Nasib Abdul (Diamond Platnumz) kuwa ni mfuasi wa kundi la Freemason.
Hata hivyo, amesema kutokana na msanii huyo kuomba radhi amemsamehe, lakini akirudia atamfanya kuwa simbi.
Gwajima aliwashukia watatu hao jana wakati wa Ibada ya Jumapili iliyofanyika katika kanisa lake lilopo Ubungo Dar es Salaam.
Akizungumzia kuhusu kutekwa kwa Ibrahim Mussa maarufu (Roma Makatoliki) wenzake, Gwajima alieleza kuwa aliyesema Roma ataonekana kabla ya Jumapili, ndiye anapaswa kueleza ni nani aliyemteka msanii huyo.
Gwajima alisema aliyevamia Studio ya Tongwe ni wale wale ambao walivamia Studio za Clouds, hivyo si jambo la kunyamazia.
“Ni nani anayeteka watu, anatumwa na nani, anafanya kwa manufaa ya nani? Wa kuniambia ninyamaze hayupo kwani nikinyamaza Mungu atainua mawe,” alisema Gwajima.
Alisema watu wengi wanaangalia hayo hawataki kusema kwa sababu yeye anasema lakini itafikia mahali radio, televisheni, mitandao na Tanzania itasema kwa sababu saa ya bwana itakuwa imefika.
“Sisi tunapambana na misukule iliyokufa sembuse wewe mtekaji ndio maana nawaambia waliovamia studio Clouds ndio wale wale waliovamia na kumteka Roma Mkatoliki,” alisema.
Alisema utekaji huo umefanywa na mtu mmoja ndio maana jeshi la polisi limetaka aulizwe ambaye alisema atapatikana kabla ya Jumapili.
“Ndugu zangu hebu mtingishe mwenzako muulize una akili hivi mtu akipotea Jumatano halafu ukawaambia watu atapatikana kabla ya Jumapili maana yake unajua alipo, una majeshi utamfuatilia alipo, umemficha wewe na lalalalalaaa huyu Bashite anaiaibisha nchi, Sirro anasema muulize yeye, tujiulize kama anawachukua atawachukua lini na saa ngapi, mtazame muambie ajiandae,” alisema.
Gwajima alienda mbali na kusema ziro kwenye makaratasi ndio inatafsiri namna ya kufikiri, kuzungumza na kutenda hivyo yanayotokea ni ushahidi tosha.
Alisema yeye hana mpango wa kuhama nchi na atakuwepo hapa kuhakikisha kuwa anazungumzia jamii ya Kitanzania ili iweze kufahamu haki zake.
Alisema habari ya mtu anaitwa Ben Sanane hadi leo haizungumzwi na hajaonekana jambo ambalo si sawa huku matukio kama hayo yakiendelea.
Gwajima alisema ni jukumu la wananchi kumuombea Rais, viongozi na wananchi kwa ujumla ili kukabiliana na changamoto zilizopo kwani hali ilivyo inatoa tafsiri mbaya kwa Rais.
“Nasisitiza kuwa ziro katika makaratasi inatafsiri namna ya kufikiri, kuzungumza na kutenda,” alisema.
Halima Mdee
Akimzungumzia Mdee, Gwajima alisema wakati wa uchaguzi wa wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), mbunge huyo alipotoka baada ya kutumia lugha chafu na kumtaka aombe radhi.
Gwajima alisema ni kweli Mbunge huyo aliudhika ila maneno ambayo ameyatoa kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai si sahihi kwani ni kiongozi wa muhimili.
“Halima ni mbunge wangu na tunaheshimiana sana ila hili alilolifanya halikubaliki kwani Spika ni mtu mkubwa sana hata kama Chadema haikutendewa vizuri ila Halima hilo jambo si sawa ni kweli uliudhika jambo halipo sawa nenda ukaombe msamaha,” alisema.
Alisema akiwa kama mbunge anapaswa kuangalia jamii inayomzunguka hata kama aliudhika anapaswa kufuata taratibu za kuonesha hasira zake, lazima aoneshe mfano kwao kwa kusema na kutenda.
Gwajima alimtaka mbunge huyo kuomba msamaha ana kama hatafanya hivyo atampiga tena kwani ndio jukumu lake kama kiongozi wa dini.
Diamond Platnumz
Aidha, alisema Msanii Diamond Platnumz ni mfuasi wa kundi la Freemason ila hatamchambua zaidi kwa ameshamwomba msamaha na yeye amemsamehe.
“Almasi ingegeuka kuwa maji taka ila nampa onyo kwani leo nilipanga nikupe video inaonesha kila kitu kuhusu kujiunga na kundi hilo la Freemason,” alisema.
Hivi karibuni Diamond alidaiwa kutoa wimbo unaoonyesha kumtetea mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam anayelumbana na Gwijima kuhusu vyeti bandia na kuweka mistari inayomzungumzia askofu huyo wa Kanisa la Ufufuo na Uzima.
Gwajima alisema mtu yoyote ambaye anasapoti vyeti feki hapaswi kuungwa mkono na mtu yoyote na kuwa iwapo Diamond akirudia tena ataweka kila kitu wazi.
Alisema Biblia hairuhusu mtu akiomba msamaha kupigwa hivyo yeye amemsamehe na kuwa akirudia hatakuwa na huruma naye.
Post a Comment
Post a Comment