Serikali imekuwa lift ya ushindi wa Tundu Lissu TLS (Tanganyika Law Society). Ilipokuwa ikikazana kumkamata, ikawa inamtengeneza kuwa mgombea wa pekee. Wagombea wengine wakawa hawatajwi. Wakafunikwa kabisa.
Kwa hali hiyo ulitarajia nini? Mabavu ni zero kama akili haishiriki vizuri kwenye vitendo.
Serikali kama walitaka kucheza michezo kumzuia Lissu walipaswa kutimia njia tofauti.
Njia ya kumkamata na kutoa vitisho vya kuifuta TLS, ilikuwa inampa promotion kubwa Lissu kwa mawakili wenzake na nchi kwa jumla.
Serikali ilitakiwa kufahamu kuwa TLS ni chama cha wasomi wenye kujitambua. Ukitumia njia ya kuwatisha lazima wakuoneshe uimara wao wa kisomi.
Pengine Lissu asingeshinda kama Serikali ingeonesha kuheshimu mawakili. Vitisho dhidi ya TLS maana yake Serikali iliamua kuwachukulia poa mawakili. Nao wameonesha uimara wao wa kisomi.
Kura nyingi za kishindo kwa Lissu kuwa Rais wa TLS, maana yake mawakili waliamua kupiga kura yenye tafsiri: "Ngoja tumpe huyo msiyemtaka tuone mtafanyaje." Hakuna tafsiri nyingine.
Inawezekana kweli Serikali ilikuwa na hoja nzuri kuzuia TLS kuvamiwa na wanasiasa na kugeuzwa jukwaa la siasa lakini ingetumia njia ya heshima kwa mawakili. Unatumiaje vitisho kwa jamii ya wasomi tena wasomi wenyewe wa sheria?
Nani hajui? Uchaguzi wa TLS mwaka huu uliondoka kutoka kuwa mchuano wa wanasheria na kuwa mchuano kati ya Serikali na Lissu. Na Lissu angeshindwa angesema ameshindwa na Serikali.
Ushindi wa Serikali ungemaanisha mawakili waliamua kuogopa Serikali ili TLS isifutwe. Je, wakili gani msomi angetaka kuitwa mwoga? Ndiyo maana mawakili wamepiga kura kuonesha hawatishiki na vitisho vyote vilivyotolewa dhidi yao na Serikali.
Hata sasa, ushindi wa Lissu unatafsiriwa kuwa Lissu ameishinda Serikali na siyo wagombea alioshindana nao kwenye uchaguzi TLS.
Rais John Magufuli na Dk Harrison Mwakyembe wamekuwa lift ya Lissu kushinda urais TLS 2017. Wamesaidia pia kuifanya TLS kuwa maarufu zaidi, maana sasa kila Mtanzania anaijua TLS ni nini.
Siku nyingine Serikali isitumie mabavu na vitisho, badala yake ijielekeze kwenye matumizi bora ya akili. Hili eneo limekuwa likiwaangusha sana.
Ndimi Luqman MALOTO
Post a Comment
Post a Comment