Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Rais Dkt John Pombe Magufuli akiwa bado yupo mkoani Dodoma, jana alipata nafasi ya kufanya kikao na wabunge wa chama hicho ambapo alizungumza mambo mbalimbali ambayo hafurahishwi nayo kama kiongozi mkuu wa chama.
Rais Magufuli alikutana na wabunge hao katika Ikulu ndogo ya Chamwino Mkoani Dodoma ambapo miongoni mwa mambo mengi aliyozungumza nao ni pamoja na kuwaambia kuwa anafahamu baadhi ya wabunge wanampinga Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Nafahamu baadhi yenu mnampinga Waziri Mkuu na mnataka aondolewa kwa kura ya kutokuwa na imani naye, naomba niwaambie kuwa hamtafanikiwa. Mimi namuunga mkono msaidizi wangu huyuo kwa asilimia 100 kwa nimejionea mwenye namna anavyoweza kufanya kazi, alisema Rais Dkt Magufuli.
Hata mkimuondoa, nikija kuteua mwingine nitamleta huyu huyu na endapo mtamkataa basi nitavunja bunge wote mrudi kwenye uchaguzi.
Mbali na hilo kiongozi huyo alitoa onyo kwa wabunge wa CCM ambao wanagawa muda wao wa kuzungumza na kuwapa wabunge wa upinzani pindi wanapokuwa kwenye vikao vya bunge. Kauli hii imekuja baada ya Mbunge wa Jimbo la Bunda (CCM), Boniface Getere kumpa dakika tano mbunge wa Serengeti (Chadema), Marwa Ryoba kutoka kwenye muda wake wa kuchangia ambao ni dakika 10.
Katika hatua nyingine Mwenyekiti Dkt Magufuli amewaambia kuwa anakerwa na baadhi ya wabunge kufifisha jitihada za serikali katika kupambana na dawa za kulevya huku akimtuhumu mbunge mmoja kutoa siri na kuzipeleka upinzani.
Kuhusu matangazo ya bunge kutokurushwa mubashara, Mwenyekiti wa CCM aliwaambia wabunge hao kuwa yeye ndio aliamua iwe hivyo kutokana na wabunge wengi kuwa wapiga porojo tu.
Kikao hicho kilichofanyika chini ya ulinzi mkali huku wabunge wakizuiwa kuingia na simu, kilihudhuriwa pia na Makamu wa Rais, Samia Suluhu, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge, Job Ndugai, Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula na Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana.
Post a Comment
Post a Comment