MWANAMUME wa miaka 45 aliyeachwa na mke akaenda kuolewa kama mke wa tisa na mganga, sasa atarejeshewa mahari na gharama ya kumsomesha.
Bw James Mayaka aliyekuwa na furaha tele baada ya Mahakama ya Rufaa mjini Kisumu kuamuru arejeshewe Sh200,000, alisema hatimaye amepata haki baada ya kesi ya miaka sita mahakamani.
Kati ya pesa atakazopata ni alizotumia kumsomesha Bi Everline Kerubo Makini katika chuo cha Ualimu cha Narok nchini Kenya, kati ya 2002 na 2004.
Mkewe huyo alikuwa amekata rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu ya Kisii mnamo Februari 2015.
Lakini majaji wa Mahakama ya Rufaa Wanjiru Karanja, Festus Azangalala na Gatembu Kairu, walisema kwamba uamuzi wa Mahakama Kuu ulikuwa sahihi.
Mahakama ya Kisii ilikuwa imeamuru Bi Makini, arejeshe Sh205,000 kama baadhi ya malipo ya mahari na karo ya chuo pamoja na riba.
Bw Mayaka ambaye ni naibu wa mwalimu mkuu wa shule moja ya upili alikuwa ameomba mahakama hiyo ya Kisii imwamuru Bi Kerubo amrejeshee Sh209,000 ambazo alikuwa amemlipia kama karo ya chuo. Pia, alitaka mahakama kumshurutisha amrejeshee Sh120,000 alizolipa kama mahari.
Hata hivyo, mahakama iliamuru Bi Kerubo arejeshe kiwango nusu kwa kila suala yaani, Sh104,000 kwa karo na Sh60,000 kwa mahari. Jumla ilikuwa ni Sh164,000.
Kiwango hicho hata hivyo kiliongezeka na kufikia 205,000 baada ya riba kujumuishwa. Uamuzi huo ulisomwa na Jaji Chrispin Nangila kwa niaba ya Jaji Ruth Sitati mnamo Februari 27, 2015.
Aliongeza kuwa angali anafuatilia kesi katika mahakama ya Nyamira inayolenga kumwezesha kuishi na watoto wake, ambao wako na umri wa miaka 13 na 11 mtawalia.
“Aliwachukua watoto wetu kwa nguvu na ningetaka nirejeshewe kisheria kwani najua wanataabika,” alisema.
Alisema Bi Kerubo huwabadilishia makao mara kwa mara kwa jamaa zake kwa sababu anazozielewa mwenyewe.
Alisema mke huyo aliacha boma lake mwaka wa 2009.
Walioana kwa mujibu wa ndoa za kitamaduni za Wakisii mwaka 2000. Walifanya ndoa rasmi mwaka wa 2004 katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Nyamira.
Bw Mayaka anasema mke huyo wa umri wa miaka 42 aliolewa na mganga mmoja katika eneo la Daraja Mbili mjini Kisii. Ni mke wa tisa wa mganga huyo.
Anasema wanaume wengi huogopa kutafuta haki wanapokandamizwa katika ndoa wakihofia kuonekana wanaume wanyonge.
“Wengine hawana ufahamu kuwa wanaweza kutafuta haki,” anasema. Bw Mayaka anasema yu tayari kuoa tena.
Chanzo:swahilihub.
KAMA ULIMIS VIDEO YA MCHEZAJI WA Ghana ALIE JIKANYAGA KWA KUWASHUKURU MUKE NA MCHEPUKO WAKE TAZAMA HAPA
Post a Comment
Post a Comment