MWANASIASA na mwanaharakati maarufu nchini, Tundu Lissu (49), ana uwezekano mkubwa wa kushinda nafasi ya urais wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS) uliopangwa kufanyika mwishoni mwa wiki hii,
Uchaguzi wa TLS ambao mwaka huu umetawaliwa na hali ya mvutano kati ya chama hicho na serikali ya Rais Dk. John Magufuli, umepangwa kufanyika mjini Arusha Jumamosi hii ya Machi 18.
Uchunguzi uliofanywa na Raia Mwema wa kuzungumza na baadhi ya mawakili, majaji wastaafu na wanasheria maarufu nchini umebaini kwamba Lissu; kwa sasa, ndiye anayepewa nafasi kubwa zaidi ya kushinda kwa sababu kubwa tatu.
Sababu hizo tatu zinazodaiwa kumbeba Lissu kwenye uchaguzi huo wa aina yake ni – dhamira ya wanachama wa TLS kuwa na chama kinachotimiza majukumu yake ipasavyo, idadi kubwa ya wapiga kura kuwa vijana ambao wanampenda Lissu na pia kutaka kuionyesha serikali kuwa chama hicho ni huru.
“ Sababu ya kwanza ni kwamba ingawa TLS ni mojawapo ya taasisi kongwe nchini, ikiwa imeanzishwa mwaka 1954, haijulikani sana miongoni mwa Watanzania.
“ Ni kama vile imelala. Lakini, kama umebaini, tangu ijulikane kwamba Lissu atawania nafasi hiyo, vyombo vya habari vinaandika na watu wanazidi kuifahamu. Tumepata picha kwamba kumbe taasisi yetu inamhitaji mtu wa aina yake,” alieleza mmoja wa wanasheria aliyezungumza na gazeti hili kwa masharti ya kutotajwa jina.
Mahojiano ya gazeti hili na mawakili kadhaa yameonyesha pia kwamba ingawa TLS ina wanachama takribani 5,000, zaidi ya nusu ni wanasheria vijana ambao wengi wao wanaelezwa kumuunga mkono Lissu, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Mnadhimu Mkuu wa chama hicho.
Wanasheria hao vijana wanaelezwa kuwa na mwelekeo wa kutaka mabadiliko makubwa ya uendeshaji wa taasisi hiyo na wanamwona Lissu kama mtu pekee anayewakilisha taswira hiyo ipasavyo.
Kubwa zaidi linalodaiwa kumsaidia Lissu ni hatua ya serikali kuonekana haimtaki Lissu, kiasi cha mmoja wa mawaziri wa Magufuli, Dk. Harrison Mwakyembe, kutishia kukifuta chama hicho endapo kitaendeshwa katika misingi ya kisiasa.
Dk. Mwakyembe ambaye ni Waziri wa Sheria na Mambo ya Katiba na pia mwanasheria kitaaluma na mwanachama wa TLS alitoa tishio hilo wakati akizungumza na ujumbe wa mawakili uliomtembelea ofisini kwake mjini Dodoma mapema mwezi huu.
“ Mimi nisingeweza kumchagua Lissu kuwa Rais wa TLS. Sidhani kama ni mtu sahihi kwa chama chetu. Lakini serikali ni kama imemsaidia apate nafasi hiyo na nadhani sasa atapata.
“ Serikali imemfuatafuata sana na sasa wanasheria wanasema enough is enough. Imetosha. Mwakyembe alisema wataifungia TLS. Naona watamchagua Lissu ili waone kama ana ubavu wa kukifunga chama hicho,” alieleza mmoja wa majaji waliozungumza na gazeti hili pasipo kutaka kutajwa majina yao.
Maelezo ya Mwakyembe kwa ujumbe wa TLS uliotembelea Dodoma ukiongozwa na Rais anayemaliza muda wake, John Seka, yalifanana na yale ya Rais Magufuli aliyoyazungumza Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa Siku ya Sheria, Magufuli alionya kwamba kuna watu wanataka kuingiza siasa kwenye uchaguzi wa TLS na kwamba serikali yake haitashirikiana na TLS inayosukumwa na upinzani.
“ Nitapata shida sana kuteua Jaji kutoka Tanganyika Law Society kama mtakuwa mnafanya mambo yenu kwa kutumiwa. Niwaambie kwamba kama mtafanya kazi zenu bila kujali maslahi ya taifa, mtashindwa,” alionya.
Mmoja wa mawakili maarufu nchini, Alex Mgongolwa, aliliambia gazeti hili juzi Jumatatu kwamba hadhani kwamba Lissu ni mgombea wa kudharauliwa katika kinyang’anyiro hicho.
“ Nadhani demography ( suala la umri) kwa sasa linampa faida mgombea anayeungwa mkono na vijana. Kwa hali ilivyo sasa, Lissu anaungwa mkono na mawakili wengi vijana ambao ndiyo wanaunda sehemu kubwa ya wapiga kura. Nadhani Lissu ana nafasi,” alisema Mgongolwa.
Kwa upande wake, wakili mwingine ambaye amewahi pia kuwa mwandishi wa habari, Aloyce Komba, alisema wapo mawakili wenye wasiwasi na Lissu lakini kuna mazingira yaliyopo sasa yanampa nafasi.
“ Siwezi kusema kwamba mimi nitampigia kura yangu Lissu lakini nasema kuna mazingira ambayo yanampa faida. Watu wanataka kuona TLS iliyo ngangari na wanadhani Lissu anaweza kuifanya hivyo.
“ Kuna suala la umri wa wapiga kura ambalo ni la muhimu. Kwenye chaguzi zote za karibuni, mgombea aliyeungwa mkono na mawakili vijana ndiye hatimaye alishinda. Kwa sasa, inaonekana upepo wa vijana uko kwa Lissu na hivyo huwezi kumdharau,” alisema wakili Komba.
Mwakyembe
Akizungumza na ujumbe huo wa TLS, Mwakyembe alisema serikali haitakuwa tayari kuvumilia wakati chama hicho kikianza kutimiza mambo yaliyosababisha kuanzishwa kwake na kujiingiza katika siasa.
“Kama wizara hatujui mwelekeo wa TLS kwa sasa, hatuwezi kuiacha TLS ikijiingiza katika siasa halafu tukawaangalia tu. Hatuna nia ya kuitawala TLS, ila tunawajibika kuwasimamia kwa kuwa sheria yenu iko chini yetu.
“Mkiharibu kwa lolote wizara ndiyo yenye wajibu wa kuwatolea maelezo katika hilo mnalotaka kulifanya sasa kuna mgongano wa maslahi, je, ninyi kama wanasheria hamkuliona au hamlioni?
“Serikali haina shida na wanachama wa TLS kuwa wanachama wa vyama vya siasa ila tatizo linakuja pale mnapotaka kuchagua viongozi ambao tayari wanazo kofia mbalimbali za uongozi ndani ya vyama vya siasa,” alisema na kuongeza:
“Hao ndio watakaobeba sura na mtazamo au mwelekeo wenu, hapo hatuwezi kukubali kwa kuwa watatenganishaje uongozi wao katika chama husika na uongozi wao ndani ya TLS, huo sasa ndio mgongano wa maslahi.
“Ndio maana mwanasheria yeyote akiingia katika utumishi wa umma uwakili wa kujitegemea anauweka pembeni ili kuepuka mgongano wa maslahi,” alisema Mbunge huyo wa Kyela.
Maelezo ya Tundu Lissu
“Mimi nina misimamo thabiti ya kutetea utawala wa sheria, utawala wa kikatiba na utawala bora. Ni mpinzani wa CCM kwa sababu hiyo. Kazi yangu bungeni imejengeka katika misingi hiyo. Kama nikichaguliwa Rais wa TLS huo ndio utakuwa msimamo wangu.
“Kwa bahati nzuri, misingi ninayoisimamia ndio pia ni malengo ya kisheria ya TLS kwa mujibu wa Sheria iliyoianzisha, yaani Sheria ya Chama cha Mawakili wa Tanganyika, Sura ya 307.
“Kwa miaka mingi, TLS imeacha kusimamia misingi hii kwa hofu ya kuwaudhi watawala. Kumekuwa na dhana kwamba tukiwa wapole basi mambo yetu yataenda vizuri. Mambo ya nchi yetu hayajaenda vizuri kwa sababu ya ukimya wa TLS.
“Na wala mambo ya mawakili walio wengi hayajaenda vizuri pamoja na kuwako ukimya huu. Nikiwa Rais wa TLS ukimya huu utaisha. Wanaotaka kuendesha nchi yetu kama mali yao binafsi, bila kujali sheria na Katiba yetu; wanaotaka kutawala bila vizingiti vya sheria na Katiba, hao ndio wanaoogopa kugombea kwangu. Je, ubunge wangu na uanasheria mkuu wangu wa Chadema utakuwaje???
“Kazi ya Rais wa TLS si full-time job (si ya kukaa ofisini kila siku), ni kazi ya muda tu. Sidhani kama Rais wa TLS ana ofisi ya kudumu pale Makao Makuu. Hata kazi ya Mwanasheria Mkuu wa Chadema si full-time job. Sina ofisi Makao Makuu ya Chadema. Kazi ya ubunge ni full-time lakini ina flexibility kubwa sana.
“Nje ya vikao vya Bunge na Kamati, mimi ndiye ninayepanga ratiba yangu. Kwa sababu hiyo, pamoja na majukumu mengi niliyo nayo, ninaamini nitapata muda wa kutekeleza majukumu ya Rais wa TLS. Wanaopiga kelele, akina Mwakyembe na Magufuli, wanaogopa si Chadema bali wanaogopa TLS yenye nguvu na inayojitambua.
“Hofu yao sio hofu ya Chadema, ni hofu kwamba wanasheria wakiamka katika umoja wao wana nguvu kubwa ajabu kwa sababu ya unique position waliyonayo kisiasa na kijamii. Kwa hiyo, kwenye uchaguzi huu wa TLS, choice iliyopo mbele ya wapiga kura si choice ya Chadema au CCM bali ni choice kati ya TLS inayotambua wajibu wake na TLS inayoogopa wajibu huo. It's between change or status quo (ni kati ya wanaotaka mabadiliko au kubaki hapa tulipo), alisema Lissu.
Wiki iliyopita, Kamati ya Uteuzi ya TLS ilitangaza majina ya wanachama watano wa chama hicho waliopitishwa kuwania urais wa chama hicho na nafasi nyingine.
Wagombea hao watano waliotangazwa kuwania nafasi hiyo ni Lissu, Francis Stolla, Victoria Mandari, Godwin Mwapongo na Lawrance Masha.
Stolla amewahi kuwa Rais wa TLS Kwa takribani vipindi viwili huku Masha akiwa amewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Nyamagana na pia Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.
Tume ya uteuzi ya TLS inaongozwa na Rais mstaafu wa TLS, Kibuta Ongwamuhana na wajumbe wengine ni Jaji Augusta Bubeshi, Kalolo Bundala, Ibrahim Bendera na Akida Modest.
Rais wa TLS ambaye amemaliza muda wake wa mwaka mmoja, Seka aliondolewa katika nafasi hiyo na kamati hiyo kwa madai ya kupoteza sifa. Ni yeye na mwenzake Nmbute Akaro ndiyo pekee waliokatwa kwenye majina hayo.
TLS imeanzishwa kwa Sheria ya Bunge Na 307 ya Mwaka 1955 iliyorasmishwa na Bunge baada ya Uhuru kupitia Sheria ya Judicature and Application of Laws Act (JALA) ya Mwaka 1961.
Post a Comment
Post a Comment