UAMUZI wa serikali kuhamishia kwenye majengo Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) baadhi ya wizara, uliibua mvutano bungeni jana,
Huku Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, akizomewa na wabunge wa upinzani aliposimama kutoa ufafanuzi kuhusu uamuzi huo.
Wiki iliyopita, serikali kupitia kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Anjela Kairuki, ilieleza kuwa baadhi ya wizara zinazohamia Dodoma kutoka Dar es Salaam, ikiwamo wizara yake iliyohamia mjini humo, zitatumia majengo ya Udom kwa muda wakati zikisubiri kujenga ofisi na makazi yake.
Makamu Mkuu wa Udom, Profesa Idris Kikula jana alisema jumla ya wizara sita zinahamia katika majengo ya chuo hicho.
Mvutano ndani ya Bunge jana uliibuka baada ya Mbunge wa Viti Maalum, Suzan Lyimo (Chadema) kutaka serikali ieleza sababu za kubadilisha miundombinu ya elimu kuwa ofisi za serikali. Mbunge huyo, akiuliza swali la nyongeza katika kipindi cha 'Maswali na Majibu' bungeni, alisema katika siku za karibuni Tanzania imepata sifa kubwa kwa kuwa na chuo kikubwa Afrika Mashariki na Kati chenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 40,000 kwa wakati mmoja.
“Leo cha kushangaza CCM imeamua kukifanya chuo cha Udom kuwa sehemu ya majengo ya serikali kwa kuleta utaratibu wa kubadili au kuchanganya majengo ya wanafunzi na wizara, maana tunachukua wanafunzi wetu kupeleka kwenye simba," alisema Lyimo.
Alihoji kama uamuzi huo ndiyo utaratibu wa kuhamia Dodoma, kwa kubadilisha miundombinu ya elimu kuwa ofisi za serikali.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Mhandisi Stella Manyanya, alisema chuo si majengo peke yake bali ni majengo, walimu na vitendea kazi vya kufundishia.
“Chuo cha Udom kilipojengwa, kilijiwekea utaratibu wa namna gani kinakua sambamba na majengo.
Kwa hiyo kwa taasisi au wizara kuhamia katika majengo haya ni kwa vile suala la muda mfupi na kwa sababu majengo hayo kulingana na utaratibu na mipango yake," alisema Mhandisi Manyanya.
Aliendelea kufafanua kuwa kwa sasa baadhi ya majengo ya Udom hayatumiki, hivyo baadhi ya wizara zimepewa ziyatumie wakati zinatafutiwa maeneo yake ya kujenga na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu(CDA) na wakikamilisha kuzipatia viwanja, kila wizara itakuwa na majengo yake katika kiwanja chake.
"Suala la kuhamia Dodoma tunaona (ni) lenye tija na litaongeza tija na kuongeza ufanisi mkubwa hasa kwa wananchi kwa sababu sasa watakuwa wanapata huduma kwa urahisi zaidi ikizingatiwa Dodoma foleni hakuna na ni makao makuu ya nchi.
Sisi, wizara tumejipanga na tutahakikisha tunahamia kwenye maeneo yetu," alieleza zaidi Naibu Waziri huyo.
Baada ya ufafanuzi huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu, (Mhagama) alisimama kutoa majibu ya nyongeza ambayo hata hivyo hayakupokewa vyema na upande wa kambi ya upinzani bungeni. Mhagama alisema nia ya serikali katika kukiendeleza chuo cha Udom ilijidhihirisha kutokana na nia njema ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutoa ukumbi wake na kubadilisha matumizi kutoka kwenye chama na kuwa chuo cha Watanzania wote.
"Kwa hatua hiyo hiyo ya nia njema ya serikali ya CCM, tunaendelea na Mpango wa Taifa na ilani ya uchaguzi ya CCM ya kuhamishia serikali Dodoma na naomba niwaambie waheshimiwa wabunge majengo yatakayotumika na serikali ni majengo ambayo serikali ya CCM ilishayajenga," alisema Mhagama huku wabunge wa chama tawala wakigonga meza kumpongeza na kutamka "CCM, CCM".
Waziri huyo alisema kuwa kwa sababu majengo yale ni mengi na yamejengwa na serikali hiyo, badala ya kuyaacha yaharibike bila ya kutumika, yatatumika na baadhi ya wizara za serikali.
"Naomba niwahakikishie waheshimiwa wabunge, majengo yale hayaingiliani na shughuli yoyote ya elimu pale chuoni na ninawahakikishia Watanzania," alisisitiza.
Mhagama alizipongeza wizara zilizohamia Dodoma na kupata hifadhi Udom kwa kuyalinda na kuyatumia majengo hayo na kuahidi kuwa serikali itaendelea kuongeza majengo hayo na uhamiaji wa serikali Dodoma uko palepale.
Wakati Waziri Mhagama akitoa ufafanuzi huo, baadhi ya wabunge wa upinzani walimzomea na wengine kuonekana dhahiri kutoridhishwa na majibu yaliyokuwa yakitolewa na serikali na kuanza kurusha vijembe dhidi yake. Mmoja wao alisikika kwenye vipaza sauti akisema
"mpeleke mwanao (Udom), mbona hujampeleka?"
Kutokana na zomeazomea na vijembe vilivyojitokeza katika kujibiwa swali hilo la nyongeza, Mwenyekiti wa Bunge, Najma Murtaza Giga, aliyekuwa akiongoza Bunge asubuhi, alipaza sauti na kuwataka wabunge waimarishe utulivu bungeni.
"Naomba heshima na utulivu ndani ya Bunge," alisema Giga akiwaonya wabunge.
KUOMBA MWONGOZO Baada ya kumalizika kwa kipindi cha 'Maswali na Majibu, Mbunge wa Iringa Mjini, Mch. Peter Msigwa (Chadema), alisimama na kuiendeleza hoja hiyo kwa kuomba mwongozo kwa Kiti cha Spika akitaka serikali itoe ufafanuzi juu ya taratibu za kielimu. Mch. Msigwa alitaka serikali ilieleze kama taratibu za kielimu nchini zinaruhusu wanafunzi wa elimu ya juu kuchanganywa na watu wengine katika maeneo yao ya kujifunzia. "Je, hii ni sera ya CCM au ni vipi?" Alihoji Msigwa wakati akijenga hoja yake.
"Sisi tunajua taratibu za elimu ya juu, hawa hawawezi kuchanganywa na hata na watu wa chini wa elimu ya msingi. "Naomba mwongozo wako Mheshimiwa Mwenyekiti, serikali ifafanue na ieleze kama kitendo chake cha kuhamishia shughuli za serikali katika eneo la chuo kikuu hakitaathiri mazingira ya kujifunzia wanafunzi wa chuo hicho."
Mbunge huyo alisema zaidi:"Udom kuna mabango kabisa yameandikwa ‘Graduate with A not AIDS’ (Hitimu kwa kupata darala A na si kwa kupata Ukimwi), lakini kwa hilo la wanafunzi kuchanganywa na watu wa kawaida, sasa watasikia wamehitimu na Ukimwi." Mch. Msigwa, ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Mambo ya Nje, alisema hajaridhishwa na majibu ya Mhagama kuhusu suala hilo la kuhamishia Udom shughuli za serikali. Hata hivyo, Mwenyekiti wa Bunge Giga, akijibu mwongozo huo, alisema majibu yaliyotolewa na Waziri Mhagama yanajitosheleza, hivyo 'kuiua' hoja ya mbunge huyo.
WATU 17 Katika hatua nyingine, Waziri wa Nchi 0fisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Anjelah Kairuki, amezindua rasmi utoaji wa huduma kwa wananchi katika ofisi yake mpya iliyopo Udom akieleza kuwa hadi jana jumla ya watu 17 tayari walikuwa wameshapatiwa huduma tangu Januari 30 walipohamia mkoani humu.
Akizungumza na waandishi wa habari na watumishi wa wizara hiyo wakati wa zoezi la uzinduzi wa ofisi ya wizara hiyo jana, Kairuki alisema uzinduzi huo ni sehemu ya kuunga mkono agizo la Rais la serikali kuhamia Dodoma. Alisema kuwa ofisi hiyo ambayo ipo katika jengo la ofisi ya Shule ya Sanaa na Sayansi za Jamii katika chuo hicho na kuwataka wananchi wote wanaohitaji huduma yao kufika katika eneo hilo. "Napenda kutumia fursa hii kuwapongeza na kuwashukuru Wakala wa Majengo (TBA) kwa kazi nzuri ya ukarabati na kuliweka jengo letu katika hali nzuri kwa kipindi cha muda mfupi ambapo inawawezesha watumishi kutoa huduma kama kawaida," alisema. Aliongeza kuwa kutokana na uhamisho huo wa ofisi, masula yanayohusu sera na sheria za utumishi wa umma na utawala wa utumishi wa umma ndiyo yatakayotekelezwa katika ofisi hiyo ya Dodoma. “Masuala ya usimamizi wa malipo ya mishahara, uendeshaji rasilimaliwatu, ukuzaji maadili, anuai za jamii, uchambuzi ushauri wa utendaji kazi na huduma ya teknolojia ya habari na mawasailiano yatashughulikiwa na ofisi yetu ya Dar es Saalam kwa sasa kwa kuwa idara hizo zimepangwa kuhamia Dodoma katika awamu ya pili na tatu," alifafanua. Makamu Mkuu wa Udom, Prof. Kikula alisema haoni tatizo kwa serikali kuweka makazi yake hapo wakati wakiendelea kujipanga kutafuta eneo ambalo litakuwa ni la kudumu kwa ajili ya serikali tofauti na ambavyo watu wamekuwa wakisema katika mitandao ya kijamii. "Watu wanadai eti muingiliano wa watumishi na serikali utaleta matukio ya vitendo vya umalaya lakini mimi kwangu naona huo ni mtazamo hasi ambao hauna tija," alisema. "Mbona (Chuo cha Usimamizi wa Fedha) IFM, (Chuo Kikuu cha Dar es Salaam) UDSM, (Chuo cha Biashara) CBE, (Chuo cha) Mipango kuna muingiliano wa watu na hakuna tabia hizo, huwezi kuzuia muingiliano wa watu hata siku moja,” alisema. Msomi huyo alizitaja wizara hizo ambazo zinatarajiwa kuweka ofisi zake katika chuo hicho kuwa ni Katiba na Sheria, Utumishi wa Umma, Viwanda na Biashara, Afya, Elimu pamoja na Mambo ya Ndani ya Nchi.
Post a Comment
Post a Comment