JUNI 23 mwaka jana, Rais John Magufuli alipokea ripoti ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 kutoka kwa Mwenyekiti (mstaafu) wa Tume ya Taifa ya uchaguzi (Nec), Jaji mstaafu Damian Lubuva.
Hafla ya kuipokea ripoti hiyo ilifanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli akazungumzia masuala tofauti ikiwapo kusitisha shughuli za kisiasa hususani mikutano ya hadhara na maandamano.
Pamoja na mambo mengine, Rais Magufuli akasema ni wakati wa ‘hapa kazi tu’, hivyo wananchi waachwe wafanye kazi pasipo kuingiliwa na masuala ya siasa, wakati Serikali yake ikitekeleza ahadi zilizotolewa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu huo.
Hoja nyingi zilitolewa kumsifu na kumpongeza Rais Magufuli kwa hatua hiyo, kama ilivyokuwa kwa wakosoaji wake walioelezea kukandamizwa kwa misingi ya demokrasia.
Lakini tangu Rais Magufuli apige marufuku mikutano ya hadhara, kisha kutolewa kwa tamko la jeshi la polisi hakuna chama ama mwanasiasa aliyekiuka maagizo hayo, isipokuwa kwa kufanya vikao vya ndani kwa chama husika.
Kutoka Juni 23, mwaka jana Rais Magufuli alipotoa tamko la kuzuia shughuli hizo za siasa, hadi Desemba 23 mwaka jana ilipoanza mikutano ya kampeni za udiwani ikawa takribani siku 30 zilizotoa mwanya kwa wanasiasa wa upinzani angalau kuwa huru kwenda sehemu tofauti za nchi wakishiriki na kuhutubia mikutano ya hadhara.
Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe akasema ulikuwa ni wakati muafaka kwa wapinzani kuzitumia kampeni hizo kwa ajili ya kuzungumza na wananchi masuala ya kitaifa, kwa vile zilipofikia ukomo wake Januari 21, mwaka huu, wangerudi kwenye ukimya kwa maana hapatakuwa na mikutano ya hadhara.
Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini kupitia chama hicho, anathibitisha kuwa agizo la Rais Magufuli na hatua ya polisi kusitisha mikutano ya hadhara ya kisiasa litaendelea kufuatwa baada ya uchaguzi wa udiwani wa marudio wa ubunge katika jimbo la Dimani kufanyika.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, akakaririwa akisema ukimya wa wapinzani unaotokana na maagizo hayo hauwaathiri wanasiasa pekee bali jamii nzima kwa vile inanyimwa uhuru wa kujieleza.
Naye Mwanasheria Mkuu wa Chadema ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu anasema kampeni za udiwani na ubunge zilitoa mwanya wa uhuru katika kufanyika kwa mikutano ya hadhara isiyoweza kuzuiwa.
Lissu ambaye kitaaluma ni mwanasheria, akasema ni kutokana na hali hiyo wanasiasa hasa wa upinzani walizitumia kampeni za uchaguzi huo kuzungumzia masuala tofauti hususani matatizo yanayolikabili Taifa.
MIKUTANO YA NDANI
Mara kadhaa, viongozi wa upinzani akiwamo aliyewahi kuwa Waziri Mkuu ambaye kwa sasa ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Ed-ward Lowassa, wamekuwa wakiisifu kuwa ni yenye kuwaimarisha na kuwajenga zaidi.
Hoja hiyo inaungwa mkono na Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro, akisema mikutano ya ndani bado inawanufaisha kwa vile inatumuka kuikosoa Serikali na ujumbe kuwafikia wananchi.
Hata hivyo, Mtatiro anaamini kuwa pamoja na katazo la Rais Magufuli na polisi kuhusu mikutano ya hadhara, mabadiliko ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano yanawawezesha (wapinzani) kufikisha ujumbe kwa jamII Pana kama inavyofanyika katika nchi nyingine duniani.
“Tunaweza hata kutumia mitandao ya kijamii na hizi kampeni za uchaguzi mdogo kufikisha ujumbe kwa umma. Sioni kama kuna njia mtu anaweza kuitumia kwa sasa kuvizuia vyama vya upinzani kuzungumzia matatizo ya wananchi,” akasema.
Lakini wapo wanasiasa wanaoamini kwamba kuwapa wapinzani fursa ya kuzungumza na kusikika kwenye jamii, kunasaidia kuyajadili na kupata mawazo mapya ya kukabiliana na kero zilizopo nchini.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa CUF, Shaweji Mketo, anasema wapinzani wanapozuiwa kutoyazungumzia matatizo ya nchi ni sawa na kuashiria kutohitaji kadhia hizo kujulikana na kusikika.
Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, akasema hakuna haja ya kuwazuia wapinzani kufanya shughuli za siasa hususani mikutano ya kampeni kwa vile baadhi ya mambo yanayotekelezwa na Serikali, yamo kwenye ilani ya uchaguzi.
Sumaye anasema masuala yaliyopo kwenye ilani ya Chadema ya mwaka jana, hayana athari kwa Taifa na ndio maana miongoni mwa hayo yanatekelezwa na Serikali ya awamu ya tano.
MIKUTANO ILIVYOZUIWA
Rais Magufuli alitoa kauli ya kupiga marufuku mikutano ya wanasiasa alipokuwa akizungumza Ikulu Dar es Salaam, baada ya kukabidhiwa ripoti ya Uchaguzi Mkuu wa 2015.
“Niwaombe wanasiasa wenzangu wafanye siasa za ushindani kwa nguvu zote baada ya miaka mitano ili wananchi watuhoji tuliyoyaahidi kama tumeyatekeleza au hatujayetekeleza,” akasema.
Rais Magufuli alisema hatua hiyo ni sahihi kwa vile hata nchi zilizobobea kwenye misingi ya demokrasia (hakuzitaja), haziendelezi siasa baada ya uchaguzi na badala yake kuwekeza katika kufanya kazi.
Akasema, “haiwezekani mkawa kila siku ni siasa watu watalima saa ngapi, kila siku ni siasa, ni vema tukatimiza wajibu wetu tuliopewa na wananchi na watatupima kwenye hilo.”
Rais Magufuli akaelezea matumaini yake kuwa Watanzania wanachokihitaji kwa wakati huu ni maendeleo.
Rais Magufuli akasema katika kampeni za 2015, aliahidi kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ndani ya kipindi cha miaka mitano, hivyo asingependa kuona mtu yeyote anamchelewesha katika utekelezaji.
USHAURI
Rais Magufuli akashauri kuwa kama kunan hitaji la kuwapo mikutano ya hadhara, isiwe kwa wanasiasa wakiwamo wabunge kutoka majimbo mengine kwenda kuungana na mbunge wa jimbo husika kuwahutubia wananchi.
Badala yake akasema kila mbunge na diwani anapaswa kufanya mkutano ndani ya eneo lake la uwakilishi. Akatoa mfano akisema, “kama ni madiwani wakapeleke hoja kwa nguvu zote kwenye maeneo yao, kama ni wabunge wakazungumze kwa nguvu sana bungeni lakini hata kuziba midomo nayo ni demokrasia, hiyo ni demokrasia ya mwelekeo wa ya aina yake.”
KUSHIRIKIANA NA WAPINZANI
Rais Magufuli akasema Serikali yake imeamua kufanya kazi kwa kushirikiana na vyama vyote vya
siasa ili kuchagiza kasi ya kutatua kero za wananchi.
Katika kuthibitisha hilo, akasema atashirikiana na wanasiasa katika changamoto ambazo utatuzi wake utasaidia kulijenga taifa.
Post a Comment
Post a Comment