Siku chache baada ya mwanamke Ruth Segeleti (52) kufukua kaburi la mtoto wake Baraka Mwafongo (22), kwa imani kwamba angefufuka baada ya siku tatu, imeelezwa kwamba alifanya hivyo akidaiwa kwamba aliota kuwa mtoto wake atakuwa nabii.
Akisimulia maisha ya mwanamke huyo, balozi wa nyumba 10 katika mtaa wa Shigamba, Shaban Anangisye alisema mzazi huyo wa watoto wane wakiwamo wa kike watatu na marehemu ambaye alikuwa mwanaume pekee, aliwaambia wanawake wenzake siku moja baada ya kumzika marehemu kwamba aliota ya kuwa mwanaye ni nabii na hajafa.
“Mtoto wake alifariki Februari 15 akiwa nyumbani na alikuja kwangu kunieleza na alitaka azikwe Februari 17, lakini mimi nilimshauri kwamba ampeleke mochwari, kama hana fedha basi azikwe Februari 16 jambo ambalo alilikubali,” alisema.
Alisema aliwaarifu majirani, lakini walisita kufika kwenye msiba huo kwa vile mwanamke huyo hakufahamika sana kutokana na ugeni wake na kushinda ndani akimuuguza mtoto wake ambaye alikuwa akiumwa tangu 2013.
Anangisye alisema majirani waliamua kuhudhuria mazishi baada ya yeye kuwaeleza ukweli kwamba tangu amehamia hapo amekuwa na magonjwa hivyo kushindwa kuhudhuria misiba ya majirani. “Watu walijitokeza kuzika na majirani walibaki kumliwaza.. lakini usiku aliwaambia kwamba mtoto wake atafufuka.”
Anangisye alisema baada ya kusimulia hayo, alidamka alfajiri kwenda kufufua kaburi na alionekana akirudi na jembe pamoja ana furushi la nguo akitokea makaburini. “Wanawake wenzake walipomwona walikwenda mbio makaburini na kuona kaburi likiwa limefukuliwa ndipo walipokuja kwangu kunieleza ili kuwataarifu polisi,” alisema.
Alisema kuwa alipiga simu polisi ambao walifika na kuomba kibali cha Mahakama kufukua kaburi hilo ambalo walikuta sanduku tupu na ilibainika baadaye kuwa mwili wa marehemu umelazwa kwenye banda la mwanamke huyo.
Anangisye alidai kwamba mwanamke huyo alikiri kufukua kaburi hilo akisaidiwa na vijana wawili aliowapa sh.5, 000 kila mmoja na kwamba alimbeba mtoto wake mgongoni hadi kwenye banda alilomweka akisubiri Mchungaji afike kumwombea ili afufuke.
Alisema baada ya maneno hayo alichukuliwa pamoja na maiti ya mwanaye hadi kituo cha polisi huku mwili wa marehemu ukipelekwa Hospitali Teule ya Ifisi.
Baada ya kuenea kwa taarifa za tukio hilo, wananchi walivamia nyumba ya mama huyo na kuichoma moto. Polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya na jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Dhahiri Kidavashari alisema watu saba wamekamatwa kwa tuhuma hizo na wapo nje kwa dhamana.
HT: MWANANCHI
Post a Comment
Post a Comment